BAADHI ya vijana wanaoendesha pikipiki maarufu bodaboda wa Kata ya Kyebitembe, Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera, wamedaiwa kuwa chanzo cha mimba za utotoni kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Mwenyekiti wa Kamati wa Afya, Elimu na Maji wa Halmashauri ya Muleba, Evati Tirwetwa, alibainisha hayo na kufafanua kuwa tangu mwaka jana hadi Aprili, mwaka huu, wanafunzi 32 wamepewa ujauzito katika wilaya hiyo huku Kata ya Kyebitembe ikiongoza kwa zaidi ya matukio 12 ya wanafunzi kupewa ujauzito.
“Watuhumiwa 17 walikuwa wanatafutwa ambapo 11, hata hivyo walalamikaji hawakutokea mahakamani na kesi zilifutwa wakati kesi tatu zinaendelea kusikilizwa na moja mtuhumiwa alihukumiwa,” alieleza.
Tirwetwa alisema baada ya kubaini ukubwa wa tatizo hilo waliunda kamati ili kujua chanzo, ambapo kesi nyingi watuhumiwa walikuwa waendesha bodaboda wanaodaiwa kuwarubuni wanafunzi wa kike kwa kuwapa lifti za kuwapeleka shuleni na kuwarudisha nyumbani.
“Lakini zipo changamoto tunazokabiliana nazo kama vile wazazi kutotoa ushirikiano pale watuhumiwa wanapokamatwa na kufikishwa mahakamani, wakati mwingine watoto wao waliofanyiwa ukatili wa kubebeshwa mimba wanawazuia wasiende kutoa ushahidi, baada ya familia kumaliza kesi hizo nyumbani,” alieleza.
Alitoa mfano kuwa wapo baadhi vijana wanatajwa kisha wanakamatwa, lakini baada ya siku kadhaa wanaachiwa kwa kukosa ushahidi wa kuwatia hatiani.
Naye, Ofisa Elimu wa halmahauri hiyo, Jered Muhile, alisema mwanafunzi anapopata mimba akiwa shuleni anaondolewa shuleni kwa mujibu wa kanuni namba nne ya kanuni za elimu ya mwaka 2002 ambayo inaelekeza kufukuzwa shule mwanafunzi yoyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya mapenzi.
Mwanafunzi aliyeacha shule baada ya kupata ujauzito, alidai alipata ujauzito akiwa kidato cha pili, baada ya kukutana na dereva bodaboda aliyemuahidi kumpatia fedha za matumizi.
Alisimulia kuwa mwaka 2019 baba yake alifariki dunia na baada ya miezi mitatu mama yake alipata ajali ya gari iliyomsababishia kivunjika viungo vya mwili na kulazwa hospitali mwaka mzima.
“Kipindi hicho nilikuwa kidato cha pili hivyo nilikosa msaada wa kupata mahitaji yangu muhimu nilijikuta naingia katika uhusiano wa kimapenzi na kijana mmoja dereva wa pikipiki, aliyeahidi kuwa atanipatia fedha za matumizi kweli alifanya hivyo, ilipofika Januari mwaka jana niligundulika kuwa mjamzito nikafukuzwa shule,” alieleza.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasindaga, Elisha Charles, alisema tatizo la wanafunzi kubeba mimba wakiwa bado shuleni linachangiwa na umbali uliopo kati ya shule na makazi yao, kwa kuwa hutembea kilometa 18 kwenda na kurudi shuleni.
Na Angela Sebastian, Bukoba



























