MADIWANI wamempongeza Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, kwa kuwakumbusha wajibu wao katika kutatua kero za wananchi na kusimamia miradi ya maendeleo katika kata zao.
Baadhi ya madiwani wakizungumza na UhuruOnline kwa nyakati tofauti, jijini Dar es Salaam, walisema Shaka amewaamsha katika utekelezaji wa majukumu yao.
Diwani wa Kata ya Tandale, Manispaa ya Kinondoni, Abdallah Said ‘Chifu’, alisema Shaka amefanya jambo jema akiwa ni msimamiaji wa utekelezaji wa Ilani ya CCM.
“Binafsi nimpongeze kwa kutukumbusha katika majukumu yetu, kama unavyofahamu, hili ndilo jukumu letu la msingi sisi madiwani na miradi mingi inafika na kutekelezwa katika kata
zetu,”alisema.
Said alisema kauli hiyo ni agizo la Chama
katika kuhakikisha madiwani wanawajibika ipasavyo katika nyadhifa zao.
Diwani huyo alisema wana wajibu wa msingi wa kuangalia iwapo miradi ya maendeleo inayotekelezwa inaendana na thamani ya fedha iliyotumika.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya 14 Temeke, Omary Babu, alisema kauli hiyo ni mwafaka kwasababu madiwani ni wawakilishi wa wananchi katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo ya kata zao.
Babu alisema kuwa mfumo wa utekelezaji wa miradi kwa sasa inafuata taratibu zote za kisheria, hivyo inakuwa rahisi kwa diwani kujua kinachoendelea katika mradi husika.
Diwani huyo alisema maelekezo hayo ya
Shaka watayatumia vyema katika kutafuta suluhu ya kero za wananchi na usimamiaji wa miradi ya maendeleo.
Shaka akiwa katika Kata ya Mbetele, Manispaa ya Songea, Ruvuma, wiki hii alisema Chama kinataka kuwaona madiwani wake nchi nzima wakifanya kazi ya kuwatumikia wananchi ikiwemo kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo.
Alisema madiwani hao wanapaswa kufanya kazi inayoendana na kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuwatumikia wananchi hususan wanyonge.
“Mimi binafsi nimpongeze kwa kutukumbusha katika majukumu yetu, kama unavyofahamu hili ndilo jukumu letu la msingi sisi madiwani na miradi mingi inafika na kutekelezwa katika kata zetu. Diwani wa Kata ya Tandale, Manispaa ya Kinondoni, Abdallah Said.
NA SIMON NYALOBI