Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya Miliki Bunifu Duniani (WIPO), Bw. Daren Tang ameitaja Tanzania kama nchi inayofanya vizuri katika masuala ya ushirikiano na Shirika hilo ikiwemo kushiriki Mafunzo maalum kwa njia ya masafa marefu yanayoandaliwa mahsusi kwa Majaji (WIPO Academy Distance Learning General Course on Intellectual Property for Judges).
Bw. Tang aliyasema hayo hivi karibuni wakati akifungua Kongamano la Kimaitaifa la Majaji linalojulikana kama ‘WIPO Intellectual Property Judges Forum’ lililofanyika Makao makuu ya Shirika hilo yaliyopo Geneva nchini Uswisi huku akikiri kuridhishwa na ushirikiano unaotolewa na Mahakama ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Uongozi wa Mahakama ya WIPO, Bi. Eun Joo Min Tanzania ni nchi ya pili kufanya vizuri katika ushiriki wa Mafunzo ya masafa marefu ambapo alieleza kuwa Misri inaongoza kwa kuwa na jumla ya Majaji 300 ikifuatiwa na Tanzania ambapo jumla ya Majaji na Mahakimu 70 wapo mbioni kuhitimu mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Taasisi hiyo.
Aidha; Bi. Eun aliitaja pia Tanzania kama nchi mojawapo inayoshiriki kuchapisha maamuzi yanayohusu miliki Bunifu yanayotolewa na Mahakama ya Tanzania kwenye mtandao wa ‘WIPO Lex Judgment Database’.
Mtandao huo ni maarufu Duniani unamilikiwa na Shirika hilo huwezesha uamuzi wa Mahakama mbalimbali kusomwa kote duniani. Nchi zingine zilizoruhusiwa kuchapisha maamuzi yanayotolewa na Mahakama za juu katika mtandao huo ni Marekani, Uingereza, Hispania, Japan, China, Jamaika, Australia, Brazil, Korea, Senegal, Togo, Misri, Chile, Gabon, Albania, Congo, Cameroon, Benin, Burkinafaso, Costa Rica na Ivory Coast.
Kongamano hilo liliwakutanisha zaidi ya Majaji 300 kutoka Nchi mbalimbali Duniani kwa dhumuni la kubadilishana uzoefu wa namna bora ya utoaji haki kwa siku mbili kuanzia tarehe 16 Novemba, 2022 hadi tarehe 17 Novemba, 2022. Mada Kuu katika kongamano hilo ilikuwa ni Akili Bandia (Artificial Intelligence) na nafasi yake katika utoaji wa uamuzi.
Mada zingine zilizowasilishwa ni pamoja na Uandishi wa Hukumu, Hataza na Teknolojia mpya (Patent and New Technology), Utoaji wa Zuio katika mazingira ya kidigitali, Haki miliki na Teknolijia mpya, nafasi ya Mahakama katika kuendeleza miliki bunifu na usimamizi wa mashauri.
Miongoni mwa watoa mada katika Kongamano hilo alikuwa, Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ambaye aliwasilisha mada kuhusu usimamizi wa mashauri na alitoa uzoefu wa Tanzania kwenye masuala ya usimamizi wa mashauri yanayohusu miliki bunifu .
Mahakama ya Tanzania ilishiriki katika Kongamano hilo kwa kuwakilishwa na jumla ya washiriki 22 wakiwemo Majaji 17 na Mahakimu watano ambapo kati ya idadi hiyo washiriki watatu waliohudhuria ana kwa ana (physically) ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (T) ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, Jaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Biashara, Mhe. Dkt. Ubena John na Hakimu Mkazi Mwandamizi ambaye pia ni Mwakilishi wa Mahakama ya Tanzania-WIPO, Mhe. Upendo Ngitiri na washiriki wengine waliohudhuria Kongamano hilo kwa njia ya mtandao (virtually).
Washiriki hao ni pamoja na Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Jaji Mkuu inayosimamia utekelezaji wa Hati ya Makubaliano kati ya Mahakama ya Tanzania na WIPO, Mhe. Barke Sehel, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Songea, Mhe. Jose Mlyambina, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agness Mgeyekwa.
Wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Sumbawanga, Mhe.Thadeo Mwenempazi, Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Kigoma, Mhe. Stephen Magoiga, Jaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Katarina Revocati Mteule, Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba, Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Mahimbali, Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Mwanza, Mhe. Lilian Itemba, Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Awamu Mbagwa, Mhe. Jaji wa mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi ,Mhe. Dkt. Theodara Mweneghoha, Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Mtwara, Mhe. Dkt. Eliamini Laltaika na Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Manyara, Mhe. Gladys Barthy,
Washiriki wengine ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu-Kanda ya Temeke, Mhe. Martha Mpaze, Hakimu Mkazi Mwandamizi ambaye pia ni Katibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Jovine Constantine, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Longido, Mhe. Mwajabu Mvungi na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Bupandwa-Mwanza, Mhe.Amri Katimba.
Ushiriki wa Majaji wa Tanzania katika kongamano ni sehemu ya utekelezaji wa Hati ya Makubaliano iliyosainiwa tarehe 05 Machi, 2021 kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la WIPO, Bw. Daren Tang na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.Wilbert Chuma.
Shirika la WIPO lilianza kushirikiana kwa karibu na Mahakama ya Tanzania tangu mwaka 2018 ambapo hivi sasa wanashirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo uandaaji wa majumuisho ya sheria na maamuzi yanayohusu miliki bunifu, uaandaji wa nyenzo za kufundishia (Training Materials) na Utatuzi wa Migogoro kwa njia usuluhishi.
Shirika hilo linashirikiana pia na Mahakama katika kuwajengea uwezo Majaji na Mahakimu katika eneo la miliki bunifu kupitia mafunzo maalum na ushiriki wa Maafisa hao wa Mahakama katika mikutano, semina na makongamano mbalimbali yanayoandaliwa na Shirika hilo.