Na CATHERINE MBIGILI, Dodoma
MAHAKAMA Kanda ya Dodoma, imemwachia huru Helena Sambo (52), aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji wakati akifanya mapenzi na mpenzi wake, Mussa Husseni.
Mshitakiwa huyo, aliyekuwa akikabiliwa na kesi hiyo yenye namba 160/2017, alidaiwa kutenda tukio hilo Agosti 11, mwaka 2016, katika Kijiji cha Msisi, Wilaya ya Bahi, mkoani hapa.
Akisoma hukumu hiyo juzi, kwenye mahakama hiyo, Jaji S.M. Kalunde, alisema baada kupitia ushahidi, mshitakiwa hana hatia ya kukutwa na kesi ya mauaji.
Akitolea ufafanuzi wa ushahidi uliotolewa na shahidi namba mbili, Binti Mteji, ambaye ni miongoni mwa mashuhuda wa tukio hilo, Jaji Kalunde, alisema mahakama imemtilia shaka shahidi huyo baada ya kuwa na shaka katika utambuzi wa mshitakiwa pamoja na kuonyesha wasiwasi.
“Uaminifu na ukweli kwa shahidi ni kitu kikubwa, lakini mwanzo baada ya kumuomba shahidi kutuonyesha mshitakiwa, alishidwa kumtambua kwa wakati huo, licha ya kumtafuta kwa muda mrefu. Alidai kwamba alimsahau kwa sababu ana matatizo ya kuugua kwa muda mrefu,”alisema Jaji huyo.
Akifafanua kuhusu ushahidi kutoka upande wa utetezi, Jaji Kalunde, alisema mahakama hutambua mshitakiwa hakuwa na nia ya kuua kwa kuangalia kama alitumia silaha gani, alishambulia maeneo gani na je, aliongea nini wakati anafanya tukio hilo.
Alieleza kuwa kwa taarifa za uchunguzi, marehemu hakuonekana kuwa na jeraha lolote, zaidi ya kuonekana kuwa na michubuko na hakukuwa na ushahidi kwamba, ilisababishwa na kitu chenye ncha kali.
Akielezea tukio hilo, Jaji Kalunde, alisema marehemu na mshitakiwa, walikuwa wapenzi tangu mwaka 2013, ambapo Agosti 11, mwaka 2016, walikubaliana wakutane mnadani.
Alisema baada ya wawili hao kukutana, walikubaliana waende kwa Binti Mteji, ambaye ni shahidi namba mbili, ambako walikuwa wakikutana siku zote kwenda kufanya mapenzi katika nyumba ya mama huyo.
“Baada ya kufika katika hiyo nyumba, walikaribishwa na kuingia katika nyumba, ambayo hukutana siku zote, wakafanya mapenzi kuanzia saa tisa alasiri hadi saa moja jioni.
“Baada ya kumaliza, marehemu alimwambia mshitakiwa tangulia kwenda msibani, ambako alikuwepo tangu mwanzo, katika kijiji jirani cha Kongogo, na kukiri kwamba alikuwa amechoka, hivyo alikuwa anapumzika kidogo,” alieleza.
Alisema baada ya kuondoka hapo, mshitakiwa hakurudi tena na kesho yake asubuhi alifuatwa msibani na polisi jamii kisha kuambiwa mpenzi wake kafariki, akihusishwa ndiye aliyefanya mauaji hayo.
Hata hivyo, alisema taarifa hizo zinakinzana na shahidi namba mbili, ambaye alidai baada ya mshitakiwa kuondoka, mita chache alimuona marehemu anatembea ndani na kudondoka mlangoni.
Alisema shahidi huyo alieleza baada ya kuona marehemu kadondoka, alimkimbilia mshitakiwa, akamwambia twende ukamuone mwezako amedondoka, ndipo mshitakiwa alipomjibu amuache asipige kelele, atakuwa sawa kwa sababu wanajuana.