WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameridhia kuongeza muda wa siku saba kwa kamati maalumu aliyoiunda kuchunguza mauaji yaliyofanyika mkoani Mtwara na Kilindi, Tanga.
Kamati hiyo iliyoanza kazi Februari 4, mwaka huu, ilipaswa kukamilisha kazi yake Februari 17, ikiwa ni siku 14 kama ilivyoelekezwa na Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa vyombo vya habari, uamuzi wa kuongeza siku hizo unatokana na ukubwa wa kazi na mahitaji ya kujiridhisha na baadhi ya masuala.
Taarifa hiyo ilibainisha kwamba kamati imeomba kuongezewa siku saba kuanzia Februari 17 hadi 23, mwaka huu.
Kamati hiyo iliundwa na Waziri Mkuu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, alilolitoa Februari 4, mwaka huu, akiwa njiani kwenda Musoma, Mara katika maadhimisho ya miaka 45 ya CCM.
Aidha, Waziri Mkuu alitoa wito kwa mamlaka husika kuendelea kutoa ushirikiano kwa kamati ili ikamilishe kazi hiyo kwa wakati na ufanisi.
Kamati hiyo iliyoanza kazi Februari 4, mwaka huu, ilihusisha wajumbe tisa kutoka taasisi mbalimbali za serikali.
Wajumbe hao ni kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Rais, TAKUKURU, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kamati hiyo iliundwa huku tayari Jeshi la Polisi likiwa limeshaunda kamati ya uchunguzi, ambapo Rais Samia alisema haiwezekani jeshi hilo lijichunguze lenyewe, ni vyema kuundwe kamati huru ya kutekeleza hilo.
Pamoja na kuundwa kwa kamati hiyo, Waziri Mkuu alimuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro, kuwasimamisha kazi Maofisa wa Polisi wa Mtwara na Kilindi ili kupisha uchunguzi wakati timu aliyoiunda ikifanya kazi yake.
Na MWANDISHI WETU



























