WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha nyingi za ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, ikiwemo wilaya ya Ruangwa, hivyo ni lazima fedha hizo zitumike kama ilivyokusudiwa.
Pia, ameagiza wenyeviti wote wa kamati za ujenzi wa miradi hiyo ikiwemo ya ujenzi wa vituo vya afya na shule, watoke katika vijiji ambavyo miradi husika inatekelezwa ili kurahisisha usimamizi wake.
Aliyasema hayo, wakati akikagua ujenzi wa shule ya Sekondari Kitandi, iliyoko Kata ya Likunja, wilayani Ruangwa, Lindi akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Lindi.
Waziri Mkuu aliwataka walioko katika kamati zinazosimamia miradi hiyo wawe waadilifu na wahakikishe wanadhibiti vitendo vya wizi katika maeneo ya miradi na ijengwe kwa viwango.
Aidha, aliongeza kuwa mpango wa Rais Samia ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma zote za kijamii ikiwemo afya, maji, umeme na barabara, ili kuwarahisishia kutekeleza shughuli zao.
“Maendeleo haya yote ni kutokana na juhudi za mkuu wa nchi, lazima tumuunge mkono, lazima tuzilinde fedha zilizotolewa na Rais wetu mpendwa.
“Kiongozi wa nchi ametoa fedha, hatuwezi kuvumilia kuona mtu mzembe katika miradi ya serikali, huu ni ujumbe kwa kamati zote zinazosimamia ujenzi wa miradi nchini,” alisema.

Kadhalika aliongeza: “Wananchi wanatarajia kuona miradi inakamilika, simamieni miradi na iishe tena kwa viwango, Rais Samia anatoa fedha kwa ajili ya miradi hii ya wananchi.”
Waziri Mkuu alisema, wajumbe wote wa kamati za ujenzi wa miradi nchini washirikishwe katika hatua zote za ujenzi ikiwemo ununuzi wa vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wake, katibu wa mradi huo Mwalimu Arafa Msuya, alisema ujenzi wa shule hiyo mpya ya sekondari ya Kitandi ambayo ni ya bweni kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, itapunguza adha ya wanafunzi wa maeneo hayo kutembea umbali mrefu hadi shule ya sekondari ya Likunja.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa imepokea sh. bilioni moja kutoka Serikali Kuu kupitia mradi wa EP4R, kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo unaojumuisha miundombinu ya majengo 16, ambayo ni jengo la utawala na majengo matano yenye vyumba 13 vya madarasa.
Miundombinu mingine ni mabweni manne yakiwemo mawili ya wanafunzi wa kike na mawili ya wanafunzi wa kiume, nyumba mbili za walimu ambazo kila moja ina uwezo wa kuhudumia familia mbili, bwalo la chakula, jiko la nje, matundu 30 ya vyoo na kichomea taka.
Na MWANDISHI WETU



























