WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, amesema Rais Samia Suluhu Hassan, amedhamiria kuboresha uhusiano wa kimataifa ili kuchochea uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi.
“Mheshimiwa Rais ameniagiza niwaambie kuwa serikali anayoiongoza ipo tayari kuwapokea, kuwasikiliza na kushirikiana nanyi katika kuimarisha shughuli za uwekezaji na biashara nchini,”alisema Majaliwa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo, alipofungua kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Waziri Mkuu amesema katika kipindi kifupi cha Rais Samia, ameboresha uhusiano na nchi mbalimbali ikiwemo Uingereza ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi.
Amesema Rais Samia ameongeza usimamizi wa sera za soko huria, sera za kiuchumi na kifedha zenye mwelekeo wa kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Amesema kwa kipindi cha mwezi Machi hadi Agosti 2021, Tanzania imeongoza kwa kuvutia kiwango kikubwa zaidi cha uwekezaji kutoka nje Afrika Mashariki ambapo kiwango cha uwekezaji kutoka nje kilifikia Dola za Marekani bilioni 2.9.
Majaliwa alisema mbali na janga la Uviko-19, Tanzania katika mwaka 2020 ilipokea uwekezaji kutoka nje wa Dola za Marekani bilioni moja na hilo limefanikiwa kutokana na juhudi za zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji.
Akizungumzia kuhusu uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Uingereza, Waziri Mkuu alisema Uingereza imeendelea kuwa mshirika wa asili wa kihistoria na muda mrefu wa kibiashara wa Tanzania.
Waziri Mkuu alitoa wito kwa mamlaka husika za pande mbili kushughulikia vikwazo vya kibiashara visivyokuwa vya kikodi, ili kurahisisha shughuli za kibiashara na huduma katika jamii bila kuathiri misingi ya ushindani.
“Uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 6.5, kutoka mwaka 2016 hadi 2020 na hivyo kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika,” alisema.
Aliongeza hivi karibuni serikali imeendelea kushuhudia uwekezaji mkubwa kutoka kwa makampuni ya Uingereza ikiwemo miradi 956 kutoka Uingereza yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 5.5, imesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania na mradi wa upanuzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero (Dola za Marekani milioni 238) na kupatikana kwa leseni ya uchimbaji wa madini ya nickel ya Kabanga.
Katika kikao hicho, Waziri Mkuu alimshukuru Mwakilishi Maalumu wa Waziri Mkuu wa Uingereza wa Masuala ya Kibiashara, Lord Walney kwa kuitangaza Tanzania kuwa sehemu sahihi ya uwekezaji na biashara hususan kwa kampuni kutoka Uingereza.
Naye, Mwakilishi Maalumu wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Walney, alisema Uingereza itaendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo na uwekezaji nchini Tanzania na wataendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali katika kukuza uchumi na uwekezaji.
Kwa Upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo alisema mkutano huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kwa kuwa unalenga kuongeza kiwango cha usafirishaji wa bidhaa kutoka Tanzania kwenda Uingereza ili kuweka usawa katika bidhaa zinazoingia na kuuzwa miongoni mwa nchi hizo mbili.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Geoffrey Mwambe, alisema lengo la kongamano hilo ni kupokea mrejesho wa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini Uingereza kuhusu mazingira ya ufanyaji wa biashara pamoja na kuboresha maeneo ambayo yana changamoto katika uwekezaji.
Aidha, Waziri Wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar, anayeshughulikia Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrick Soraga, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Uingereza kuwekeza katika sera ya Uchumi wa Bluu ambapo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetengeneza mazingira bora ya uwekezaji kwa wawekezaji hususan katika sera ya uchumi wa buluu.
Na Mwandishi Wetu