Na WILLIAM SHECHAMBO
MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Elifas Bisanda, ni miongoni mwa wanazuoni nchini, ambao wanamlilia aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli, aliyepoteza maisha Machi 17, mwaka huu, katika hospitali ya Mzena ya Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na tovuti hii, kuhusu msiba huo, anasema haubebeki kwa kuwa kiongozi huyo ambaye alikuwa mwanafunzi wake (Utahini ngazi ya Shahada ya Uzamivu), kiongozi mtumishi aliyetukuka na mtu mwenye utu na upendo kwa nchi wa watu wake.
Awali ya yote Profesa Bisanda ametoa pole kwa Watanzania wote, mke wa Dk. Magufuli, Mama Janet Magufuli, familia, Rais Samia Suluhu Hassan, ndugu jamaa na marafiki wote, kutokana na msiba huo mkubwa uliolikumba Taifa na kumuomba Mwenyezi Mungu ampokee Dk. Magufuli na kumuweka mahali pema peponi.
Profesa Bisanda anaeleza kwamba ni huzuni kubwa kumpoteza kiongozi shupavu Rais wa tano wa Tanzania, Dk. Magufuli; mzalendo, mtumishi, mnyenyekevu na mtetezi wa Wanyonge, mwingi wa huruma na mpenda maendeleo.
Anasema si jambo rahisi kueleza wema wa Dk. Magufuli mtu akaumaliza kwa kuwa amefanya mambo mengi makubwa tangu akiwa Mtumishi wa umma katika fani ya ualimu, mbunge na waziri na baadaye Rais wa nchi.