MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA), Profesa Faustine Bee, amezitaka mamlaka za maji kudhibiti upotevu wa maji ili kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo na ukusanyaji wa mapato.
Alisema mambo hayo yakifanyika kikamilifu yatasaidia kuwezesha mamlaka hizo kujiendesha zenyewe bila usimamizi wa DUWASA.
Kauli hiyo aliitoa hivi karibuni wakati bodi hiyo ilipotembelea Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mpwapwa (MPWUWSA) na Mamlaka wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Kibaigwa (KIBAWASA) na kukagua miradi ya uchimbaji wa visima inayoendelea.
“Tunahitaji kufanya uwekezaji zaidi, ongezeni ubunifu wa namna ya kupambana na upotevu wa maji, kukusanya mapato na kuandika maandiko ya miradi inayohitaji ufadhili,” alisema.
Alisema sehemu kubwa inayochangia upotevu wa maji ni uchakavu wa miundombinu na wizi wa maji, hivyo kunahitajika kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kufikisha huduma bora na haraka kwa wananchi.
”Tutoke katika asilimia 69 tulipo tufike asilimia 100 katika kuwafikishia huduma ya maji, kila mwananchi anufaike, lengo letu ni kumtua mama ndoo kichwani, kama haya yatafanyika ipasavyo sioni sababu ya nyie kuwa chini ya usimamizi wa DUWASA, mnatakiwa kuwa mamlaka kamili inayojitegemea,” alisema.
Alisema lengo la DUWASA ni kuwa mamlaka bora nchini, hivyo wameanza kuboresha uwekezaji katika usafi wa mazingira kwa kuwa hivi sasa eneo hilo halifanyi vizuri na kuzitaka MPWUWSA na KIBAWASA kuanza kufikiria namna ya kujenga mtandao wa majitaka na kutafuta maeneo ya kujenga mabwawa ya kutibu na kuhifadhi maji.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa MPWUWSA, Mhandisi Peter Kabelwa, alisema baada ya miaka mitatu mamlaka hiyo itakuwa inajitegemea baada ya kufanyia kazi masuala muhimu, upanuzi wa mtandao wa majisafi na kuongeza uzalishaji kwa kujichimba visima vikubwa vya maji.
Alisema changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo uchakavu wa miundombinu katika vyanzo vya maji vya Mayawile na Kwamdyanga, ambavyo viko katika hatari ya kuchukuliwa na maji hasa eneo la Kikombo.
Katika kudhibiti uharibifu katika chanzo hicho Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, aliitaka MPWUWSA kuandaa bajeti na kuiwasilisha kwa bodi ya wakurugenzi wa DUWASA ili ujenzi ufanyike haraka kabla mvua hazijaanza na kuepusha athari kwa chanzo hicho kutoweka.
MPWUWSA ina mtandao wa maji wenye urefu wa kilomita 58.1, matanki ya kuhifadhia maji manne yenye ujazo wa lita milioni 2 huku ikihudumia kata tatu ambazo ni Mpwapwa Mjini, Vingh’awe na Mazae ikiwa na jumla ya wateja 3466.
Bodi ya Wakurugenzi DUWASA iliitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kibaigwa (KIBAWASA) kupitia wataalamu wake kuongeza ubunifu katika ukusanyaji wa mapato, kupata wafadhili na kushirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha inafikisha huduma ya maji kwa urahisi kwa wakazi wa Kibaigwa.
Naye, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dk. Fatuma Mganga ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, aliitaka Mamlaka kupunguza gharama za uendeshaji na kujipanga kwa ujio wa mitambo ya uchimbaji wa visima na mabwawa ili kuongeza uzalishaji wa maji kwa kiasi kikubwa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji KIBAWASA, Mhandisi Oscar Bakari alisema sh. milioni 950 walizopatiwa na Wizara ya Maji wameweka pampu na miundombinu mingine katika visima vilivyokuwa havina miundombuni.
Pia kutanua mtandao wa maji mji wa Kibaigwa kwa urefu wa kilomita 7.8 na Ndurugumi kwa urefu wa kilomita 23 na mpango uliopo ni kuchimba visima vingine vikubwa vinne.
Na Halima Kambi, DODOMA



























