VIONGOZI waandamizi wastaafu na wanasiasa wakongwe nchini, Philip Mangula na Jaji Mstaafu Joseph Warioba, wamesisitiza umuhimu wa maridhiano katika taifa ili kujihakikishia fursa ya kusonga mbele kimaendeleo.
Pia, wamesisitiza umoja wa kitaifa, kuondoa viashiria vya uvunjifu wa amani na kuzingatiwa maoni ya wananchi katika mchakato wa katiba mpya.
Viongozi hao walisema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakitoa maoni mbele ya Kikosi Kazi cha Rais Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoa maoni kwa kikosi hicho, Mangula ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, alisema maridhiano ni muhimu kwa sababu yanaleta umoja, amani na utulivu nchini.
Alisema hakuna mgogoro usiokuwa na jibu, hasa wahusika wanapokaa mezani kwa ajili ya mazungumzo ya pamoja kutafuta maridhiano.
Mangula alisema mwaka 2001 kulikuwa na mgogoro kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na chama cha CUF, lakini walikaa katika meza moja kwa ajili ya maridhiano na iliwezekana ingawa ilichukua muda mrefu.
“Hakuna linaloshindikana mbele ya meza moja, meza ndiyo kila kitu, lakini mkiendelea kununiana na kila mtu akaweka fundo moyoni jibu lake ni kuliingiza taifa matatani,” alisema Mangula.
Akizungumzia katiba mpya, alisema ni mwongozo ambao upo tangu kale, lakini hupitiwa na kuwekwa katika namna yenye kuzingatia mahitaji ya wakati uliopo.
Mangula alisema katiba ya kwanza ilitengenezwa mwaka 1961 ikibeba dhamira na mazingira ya kupigania uhuru, lakini mwaka 1965 kulikuwa na katiba ya muda, katiba ya chama kimoja na sasa inajadiliwa katiba itakayoendana na mfumo wa vyama vingi vya siasa katika uendeshaji wa nchi kwa maridhiano.
“Kila mtu anahitaji katiba mpya ilimradi ilete amani, maendeleo na maridhiano ya pamoja,” alisema.
Kwa upande wake, Jaji Warioba ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, alisema amani na umoja ni vitu muhimu katika nchi.
Alisema anaona viashiria vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani ya nchi, hivyo kuwataka wananchi kuhakikisha wanaviondoa kwa maridhiano.
Jaji Warioba alisema waasisi wa taifa walijenga na kuondoa mambo yote ambayo yangewatenganisha Watanzania, kuchochea uhasama na kuvunja amani ya nchi.
Na REHEMA MAIGALA