MAONYESHO YA VYUO VIKUU 15 NJE YA NCHI KUFANYIKA ARUSHA
Na Mwandishi (Uelekeo gazeti)
VYUO 15 kutoka nje ya nchi vinatarajiwa kushiriki maonyesho yanatotarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi jijini Arusha.
Maonyesho hayo ya siku moja yatafanyika Julai 27,mwaka huu katika hoteli ya Four point by Sheraton Hoteli zamani ikijulikana kama New Arusha.
Mkurugenzi wa Global Education Link (GEL), Abdulmalik Mollel, alisema walianza kufanya maonyesho Zanzibar kuanzia Julai 15 hadi 21, mwaka huu na mahitaji yamekuwa makubwa kwa wanafunzi.
Zanzibar GEL ilifanya maonyesho mengine jijini Dar es Salaam lakini kutokana na mahitaji kuwa makubwa kwenye mikoa mingine wameandaa mengine Arusha.
“Maonyesho Zanzibar yalifana sana na wanafunzi wamekuwa wengi kwa hiyo tulipoona mahitaji yamekuwa makubwa tumeona tufanye na Arusha siku ya Jumamosi ili wanafunzi wengi wapate fursa ya masomo,” alisema
Alisema mwanafunzi atakayeshiriki kwenye maonyesho hayo atapata taarifa zote kuhusu vyuo vikuu nje ya nchi na atakaye taka kudahiliwa atapata udahili hapo hapo.
“Wanafunzi, wazazi na walezi watumie fursa hii kukutana na wawakilishi wa vyuo vikuu vya nje ya nchi kutoka nchi za Uingereza, Canada, India, Cyprus, China Iran na vingine vingi vitashiriki kwa hiyo wanafunzi waje kwa wingi tutafungua maonyesho saa tatu na tutayafunga jioni kwa hiyo tukutane Arusha,” alisema
Meneja wa (GEL)Regina Lema alisema wamekuwa na kampeni ya muda mrefu ya maonyesho ya vyuo vikuuu nje ya nchi ambapo walianzia visiwani Zanzibar.
“Napenda kuwakaribisha wakazi wa kanda ya kaskazini kuja kwenye maonyesho ya vyuo vikuu vya nje ya nchi ili waone fursa mbalimbali zinazopatikana na kutakuwa na udahili wa hapo hapo kwa watakaohitaji kusoma nje ya nchi,” alisema Lema
“Kutakuwa na vyuo vikuu 15 vya nje ya nchi na kutakuwa na fursa ya ufadhili wa asilimia 100 kwa vyuo vikuu vya Irani kwa hiyo sisi GEL tunaona hii ni fursa adimu ambayo wanafunzi wote wanapaswa kuitumia,” alisema.
Aidha, alisema walianza maonyesho hayo Zanzibar kuanzia tarehe 15 mpaka 21 mwezi huu na tarehe 23 na 24 maonyesho kama hayo yalifanyika katika hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.
“Huu ni mwendelezo wa maonyesho ya vyuo vikuu nje ya nchi, tulianza Zanzibar, tukaja Dar es Salaam na sasa tunaelekea Arusha siku ya Jumamosi pale Four point by Sheraton hii ni fursa kubwa siyo ya kukosa,” alisema