SERIKALI imesema mapato ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli Jijini Dar es Salaam, yameongezeka kutoka 500,000 hadi kufikia 1,195,000 kwa siku.
Ongezeko hilo limetokana na idadi ya mabasi yanayoingia na kutoka stendi hiyo kuongezeka kutoka 100 hadi 265 kwa siku.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ilisema ongezeko hilo limetokana na matokeo ya agizo la Waziri wa wizara hiyo, Innocent Bashungwa, alililolitoa Mei 30 mwaka huu kwa kuyataka mabasi yote kuingia kituoni.
“Ongezeko hili limetokana na agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Innocent Bashungwa alipofanya ziara yake Mei 30 2022,na kuagiza mabasi yote kushusha na kupakia abiria katika stendi hiyo na sio kinyume na hapo,”ilisema.
Mei 30, mwaka huu, akiwa kituoni hapo Bashungwa alitoa siku saba kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla kukaa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) pamoja Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kuyachukulia hatua mabasi ambayo hayaingi ndani ya kituo hicho.
Bashungwa alisema kwa mwezi kituo hicho hupoteza sh.miilioni 58 kutokana na mabasi hayo kutokuingia ndani, huku kiasi cha sh.bilioni 4.3 kikielezwa kukusanywa tangu kituo hicho kuanza kufanya kazi mwaka jana.
Agizo la Waziri Bashungwa kwa mkuu wa mkoa, lilikuja kufuatia kauli ya Mbunge wa Jimbo la Kibamba Issa Mtemvu kueleza kuwa, yapo mabasi hayaingii katika kituo hicho hali inayowakosesha fursa wajasiriamali na mapato katika Halmashauri.
“Yapo mabasi yanakataa kuingia ndani hili ni tatizo,hawa watu ni wakubwa na kuna maneno nasikia watu wanasema sisi viongozi hatuna uwezo wa kuwafanya waingie ndani,”alisema Mtemvu.
Waziri Bashungwa alisema kwa kuwa changamoto hiyo iliwasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, kwa kipindi kirefu na hadi sasa hakutoa ufumbuzi, alimpa siku saba kuhakikisha anapata ufumbuzi wa changamoto hiyo.
‘’Kwasababu alipelekewa changamoto hii na ameshaanza,nimpe siku saba kukaa na TABOA,LATRA kuangalia utaratibu wa mabasi kuingia na kushusha abiria ndani, jambo hili litekelezwe na lisimamiwe, ujenzi wa kituo hiki tumetumia sh.bilioni 50 na maboresho yanaendelea,”alisema.
Na MWANDISHI WETU