Na Happiness Mtweve, Dodoma
MTENDAJI Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), Justina Mashiba, amewaongoza watendaji wa mfuko huo katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani kwa kutoa msaada wa vitu mbalimbali vinavyogharimu Sh. Milion 4.5 katika kituo cha watoto wenye uhitaji cha Nyumba ya matumaini eneo la Miyuji jijini Dodoma.
Justina akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo hufikia kilele chake Machi 8 kila mwaka mfuko huo umeona ni vyema ufanye Maadhimisho hayo kwa namna ya tofauti ya kusaidia watu wenye mahitaji maalum.
“Kama taasisi tumeona ni vyema tuadhimishe siku hii ya wanawake nami nikiwa ni mwanamke ninayeongoza taasisi hii, ni siku yetu muhimu ya kutambua mchango wa mwanamke na thamani ya mwanamke katika jamii, mama ndio mlezi wa familia, tumeona tutoe msaada wa mahitaji mbalimbali zinazotelewa katika kituo hiki cha nyumba ya matumaini kinacholea watoto wenye mahitaji(yatima),” Justina Mashiba
Mkuu huyo UCSAF amesema wao ni wazazi hivyo wanawajibu mkubwa wa kuwahudumia watoto wao bila kujali wamewazaa ama hawajawazaa, watanzania wote ni ndugu ni familia moja hivyo ni lazima kusifiana bila kubaguana kwa ramgi, dini wala kabila.
“Kwa kuliona hili tuliona ni vyema watendaji wa mfuko tukusanyane kwa pamoja hususani Wanawake ambao ndio wenye wiki yetu tuitumie kuonyesha upendo kwa watu wenye uhitaji ndio mana tukaamua kuja katika kituo hiki kuwapatia kile ambacho Mungu ametubariki kukipata,”amesisitiza Justina.
Justina ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa jamii akiwataka Kujenga utaratibu wa kutembelea watu wenye mahitaji ili kuonyesha upendo mana nao wanahitaji kupendwa na kuthaminiwa kama watoto walioko majumbani ikiwa ni pamoja na kuwasaidia chochote watakachokuwa wamebarikiwa kwa wakati huo.
Amewasii Wanawake kuacha vitendo vya ukatili kwa watoto ambavyo vimeonekana kukithiri katika jamii.
“Wanawake sisi tunapaswa kuwa mfano bora katika malezi bora na makuzi ya watoto wetu katika jamii, kuonya kwa upole na hekima, tuache vitendo vya ukatili dhidi ya watoto haipendezi kabisa tunaharibu aifa yetu bure, mtoto si lazima aonywe kwa kuathibiwa bila huruma au utaratibu,” amesisitiza Justina.
Awali akipokea msaada huo, Mlezi wa Kituo hicho cha Nyumba ya Matumaini, Sista Olea Kyala, amesema wamekuwa akikabiliwa na changamoto mbalimbali kituoni hapo katika malezi ya watoto wanaowapokea na kuwalea Kutokana na kuwa na mahitaji mbalimbali ikiwemo chakula.
Sista Olea ameishukuru taasisi hiyo kwa moyo upendo na kujitoa kwa ajili ya wengine huku akiwataka kutoishia hapo na badala yake waendelee kuwasaidia kadri Mungu atakavyokuwa akiwabariki siku hadi siku.
“Tunamshukuru Mungu na tunawashukuru sana kwa kujitoa kwenu mana tumekuwa tukipokea misaada kutoka kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya Dodoma wanapo kuja kituoni hapa hujitolea kwa hali na mali katika kuzitatua baadhi ya changamoto zinazotukabili,”amesema Sista Olea.
Mfuko huo ulikabidhi kwa uongozi wa kituo hicho msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo chakula, mafuta, na mahitaji mengine ya kike na kiume vyote vikiwa na thamani ya Sh.milioni 4.5.