MKAZI wa Bunju B, Kinondoni Dar es Salaam, Abas Abas (22), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, kujibu mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kukutwa na bangi.
Wakili wa Serikali, Benson Mwaitenda, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Sifa Jacob, kuwa mshitakiwa alitenda makosa hayo, Julai 10, mwaka huu, eneo la Bunju B, Kinondoni.
Ilidaiwa mshitakiwa siku hiyo aliiba fedha taslimu sh.30,000 na simu yenye thamani ya sh.25,000, mali ya Kennedy Charles.
Mshitakiwa huyo anadaiwa kabla na baada ya kutenda kosa hilo, alimtishia Charles kwa panga.
Katika shtaka la pili, mshitakiwa huyo alidaiwa siku hiyo, eneo la Mabwepande, Kinondoni alikutwa na dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa gramu 15.75.
Mshitakiwa alikana kutenda makosa hayo, ambapo upande wa Jamuhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Mshitakiwa alirudishwa rumande kwa kuwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Hakimu alitoa masharti ya dhamana kwa kosa la kukutwa na bangi ambayo ni mshitakiwa awe na mdhamini atakayetia saini dhamana ya sh.milioni moja. Kesi iliahirishwa hadi Septemba 22, mwaka huu.
EVODIA MICHAEL( UDSM) NA HAWA NGADALA



























