STRAIKA mahiri wa Yanga, Fiston Mayele, amesema kuipita Simba alama 10 hakutowafanya wapunguze kasi ya kuwania ushindi katika mechi zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mayele anayeshika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora hadi sasa, akiwa na mabao sita, amesema Yanga bado ina mechi nyingi ngumu zilizobaki, hivyo kuongoza ligi hakutowafanya wabweteke.
Staa huyo kipenzi cha Wanayanga amesema kuwa, akisaidiana na wenzake kikosini, atahakikisha timu inavuna alama tatu katika kila mechi ili izidi kujikita kileleni na kuwa na uhakika wa kutwaa taji.
Amesema faida ya Yanga kuwa juu kwa pointi nyingi hakutawafanya waridhike kwani ligi ya msimu huu haitabiriki na wapinzani wao wanaweza kufanya lolote katika michezo yao.
“Malengo ya timu yangu yanabaki pale pale, kushinda na kupata alama tatu ndio wimbo wetu wa kila siku mazoezini na katika vyumba vya mapumziko, tuna kila sababu ya kutimiza ndoto za mashabiki wetu msimu huu,” alitamba Mayele.
Winga Dickson Ambundo, ambaye alifunga bao pekee la ushindi wa 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania juzi, alisema bao alilofunga lilitokana na maelekezo ya kocha, Nasreddine Nabi.
“Nilifunga bao baada ya kupata maelekezo ya kocha, ilikuwa ni lazima tupate pointi tatu katika mechi hiyo na ninaamini tutavuna pointi nyingi zaidi katika michezo ijayo,” alisema Ambundo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, alisema matunda ya kufanya vyema msimu huu yanatokana na uwekezaji bora wa wachezaji na benchi la ufundi.
“Wachezaji wanapambana, lakini viongozi tunatimiza wajibu wetu wa kuihudumia timu katika Nyanja tofauti huku benchi la ufundi nalo likitimiza majukumu yake kwa asilimia kubwa,” alisema.
Na ABDUL DUNIA