MKAZI wa Kata ya Ilunde, Tarafa ya Inyonga, Wilaya ya Mlele, Mkoa wa Katavi, Seda Mbuta (47), anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na nyara za serikali.
Nyara hizo ni mafuta ya simba, ngozi ya kakakuona, ngozi ya paka pori, ngozi ya simba, vipande vinne vya meno ya ngiri na mkia wa nyumbu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Katavi, ACP Ali Makame Hamad, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Novemba 23, mwaka huu, saa tisa alasiri, katika pori la akiba Rungwa, lililopo Kata ya Ilunde, Wilaya ya Mlele.
Alisema mtuhumiwa bado anashikiliwa na polisi kwa upelelezi zaidi na atafikishwa mahakamani pindi ushahidi utakapokamilika.
Katika hatua nyingine, Kamanda Hamad aliwasisitiza wananchi Mkoa wa Katavi wanaomiliki silaha kinyume na sheria kuendelea kuzisalimisha silaha hizo kwa kipindi hiki cha msamaha uliotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
“Kwa wale wote watakaozisalimisha silaha zao ndani ya muda uliotolewa, watapewa msamaha wa kutoshitakiwa, hivyo wazisalimishe katika vituo vya polisi, ofisi za serikali za mitaa na ofisi za watendaji kata,”alisisitiza.
Alieleza kuwa baada ya muda huo kukamilika, alisema wataendesha oparesheni ya kuwasaka wale wote waliokaidi kusalimisha silaha zao kwa wakati.
Na Irene Temu, Katavi