POLISI Mkoa wa Songwe, inamshikilia Shukrani Kamwela (20) kwa tuhuma za kumuua Subira Kibona (16) waliyekuwa wakiishi kama mke na mume, ambaye ni mjamzito kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali na kisha kumchoma moto.
Akizungumza na UHURU, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, ACP Janeth Magomi, amesema Subira alipotea Januari 13, mwaka huu na mwili wake kupatikana Januari 16, mwaka huu, katika korongo ukiwa umechomwa moto.
“Jeshi lilipata taarifa ya kupotea kwa Subira Januari 13, mwaka huu na kuanza kufuatilia, baada ya Subira kutokuonekana tangu Januari 13, mwaka huu,” alisema.
ACP Janeth alisema wananchi walifanya juhudi za kumtafuta na kuukuta mwili wake katika moja ya pori huku ukiwa umechomwa na kitu chenye ncha kali mgongoni na kuchomwa moto na kutupwa katika korongo.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, mwili wa Subira ulipatikana Januari 16, mwaka huu, ambapo inadaiwa Kamwela alimwambia msichana huyo ambaye alikuwa mjamzito waende kwa mganga wa kienyeji kutafuta dawa ya tumbo maarufu kama kata kamba.
Alisema inadaiwa dawa hiyo inasaidia mjamzito kujifungua salama, kwa kuwa Subira alikuwa na ujauzito wa miezi saba na alikataa kwenda kwa mganga huyo.
Na Mwandishi Wetu



























