SERIKALI imesema tume iliyoundwa kuchunguza sakata la kuvuja mitihani ya uuguzi ngazi ya stashahada, itawasilisha taarifa ya uchunguzi Jumatatu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, aliyasema hayo Oktoba 26, 2021, mkoani Morogoro alipokuwa akizindua majengo ya kituo cha elimu ya masafa Morogoro (CDE).
Alisema taarifa ya awali, inaonyesha ni kweli kulikuwa na udanganyifu uliofanywa na baadhi ya maofisa kwa kuvujisha mtihani huo.
“Tume tuliyoiunda inakaribia kukamilika uchunguzi wake, hivi karibuni itanikabidhi na nataka niwahahakishie wale waliohusika na tuhuma hizi, tutawachukulia hatua za kinidhamu.
Aliongeza kuwa: “Kwa sababu wao wametuongezea kazi zisizostahili na sisi kama serikali tutawaongezea kazi inayostahili kwa mujibu wa sheria, kwa sababu ripoti ya awali inaonyesha kuna uzembe ulifanyika.”
Akizungumzia umuhimu wa kituo cha elimu ya masafa, Waziri Dorothy alisema uwepo wa kituo hicho umekuwa msaada kwa watumishi wanaotaka kujiendeleza hasa katika kuwapunguzia gharama.
Aliwataka waganga wafawidhi na waganga wakuu wa mikoa, kutambua umuhimu wa chuo hicho na kuwaruhusu watumishi wao kujiendeleza kupitia kituo hicho.
“Kituo hiki kitasaidia watumishi wa sekta ya afya kujiendeleza wakiwa katika maeneo yao ya kazi bila kutoka kwenda chuo na itasaidia kupunguza gharama kwa sababu mtumishi atabaki katika eneo lake,” alieleza.
Awali, Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara ya Afya, Dk. Saitore Laizer, alisema kituo hicho kimegharimu dola milioni tatu hadi kukamilika kwake, ikijumuisha miundombunu yote ya kufundishia.
Alisema lengo la uwepo wa kito hicho ni kuwajengea uwezo wa elimu ya masafa watumishi wa afya ili kutoa huduma bora kwa wananchi, kama ilivyodhamira ya Serikali ya Awamu ya Aita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Naye, Mkuu wa kituo hicho, Profesa Ndemetier Verman, alisema kituo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa watumishi wa tehama ambapo kwa sasa wapo wawili ambao wanafanya kazi kwa mkataba.
NA LATIFA GANZEL, MOROGORO



























