MBUNGE wa Nanyamba, Abdallah Chikota (CCM), ameitaka Serikali kuweka vivutio maalum katika Bandari ya Mtwara ili kuvutia wasafirisha mizigo ya nchi za Msumbiji, Malawi na Zambia.
Katika swali lake, alihoji, Serikali imeweka vivutio gani maalum ili kuvutia wasafirishaji kutumia Bandari ya Mtwara kusafirisha mizigo yao nchi za Msumbiji, Malawi na Zambia?.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, alisema katika hatua za awali za kuvutia wasafirishaji kutumia Bandari ya Mtwara, Serikali imepunguza asilimia 30 ya gharama za tozo za bandari kwa shehena ya Korosho.
Alisema gharama hizo zinahusisha kupanga na kupokea shehena kwenda au kutoka melini (shore-handling), usafiri wa kati wa kusafirisha bidhaa kutoka melini hadi kwenye eneo la kuhifadhia mizigo na kinyume chake, kupokea na kupeleka mizigo kutoka kwenye mabehewa au malori kwenda melini; na upakuaji na uhifadhi wa mizigo kutoka kwenye meli (steve-doring).
Aidha, Serikali imetoa punguzo la ada inayotozwa kwa matumizi ya gati kushusha mizigo ndani ya meli (wharfage) kutoka Dola za Kimarekani (USD 1) hadi Dola za Kimarekani (USD 0.5), na kurefusha muda wa makasha ya kupakia Korosho kuwa bure katika msimu wote wa korosho.
Vile vile, alisema Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeendelea kutoa punguzo la tozo maalum kwa wasafirishaji wa makaa ya mawe na saruji ili kuifanya Bandari ya Mtwara kufanya kazi katika kipindi chote cha mwaka.
“Serikali itaendelea kufanya tathmini na kuchukua hatua stahiki kwa lengo la kuvutia matumizi ya bandari ya Mtwara.
napenda kutoa wito kwa wasafirishaji kutumia punguzo hili la tozo lililofanywa na Serikali kusafirisha mizigo ya nchi za Msumbiji, Malawi na Zambia kupitia Bandari ya Mtwara,”alisema.
Na MWANDISHI WETU, DODOMA