ALIYEKUWA mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kupitia chama cha ACT- Wazalendo, Bernard Membe, ameeleza sababu zilizomfanya arejee Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwemo kukitumikia Chama hicho hadi kufa kwake.
Pia, amesema uamuzi wa kumuondolea uanachama wake ni jambo lililomuumiza kwa kiasi kikubwa kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi ndio Chama alichokulia na kumuwezesha kushika nafasi mbalimbali za kichama na kiserikali, hivyo ameahidi kufia ndani ya CCM
Membe, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika serikali ya awamu ya nne, alirejea rasmi CCM, Mei 29, 2022, na kupokelewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka.
Katika mkutano huo wa hadhara ulioitishwa na Mbunge wa Mtama,Nape Nnauye, ambaye pia ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ulifanyika kijiji cha Rondo, Kata ya Chiponda, Jimbo la Mtama mkoani Lindi na kuhudhuria na mamia ya wananchi na wanaCCM.
Akizungumza katika mkutano huo, Membe alisema kurejea kwake CCM kunatokana na dhamira aliyokuwa nayo ya kukitumikia Chama hadi kufa kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi ndio chama imara chenye sera safi za kuleta maendeleo nchini.
Membe alisema Machi 30 hadi Aprili mosi, mwaka huu, aliitwa Dodoma, katika Mkutano wa Kamati Kuu ya Maadili na Mkutano Mkuu wa Halmashauri Kuu, alipewa nafasi na Mwenyekiti wa CCM Taifa kuzungumza na wanaCCM.
“Mama yetu, Rais wetu na Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa, alinipa nafasi ya kuzungumza na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama Taifa. Nashukuru kwa kupewa nafasi ile na wajumbe waliliridhia kwa kauli moja nirejee CCM.
“Nimerejea CCM kwa sababu kuu mbili, sababu ya kwanza nilishauriwa na viongozi wa dini zote, nilishauriwa na viongozi wa CCM ngazi ya wilaya na mkoa, nilishauriwa na marafiki zangu wote nirejee CCM, nilishauriwa na wanaCCM’’ alisema.
Aliongeza:“Kutokana na ushauri wote huo sikuwa na namna nyingine zaidi ya kutii, nimekubaliana na ushauri wa wote waliosema nirudi CCM na sasa nimerudi CCM,” alisema Membe wakati akitangaza kurejea tena katika Chama.
Kwa mujibu wa Membe sababu ya pili ya kurudi katika Chama inatokana na dhamira yake ya kukitumikia Chama Cha Mapinduzi hadi atakapokwenda kaburini.
“Nilipoondolewa CCM nilisikitika sana, nilisonekana sana na ninyi wananchi mlisikitika, mlisononeka. Sababu ambazo zilinifanya niondoke CCM haziko tena, narudi sababu zilizoniondoa CCM haziko tena. Nimerudi, namshukuru Mwenyekiti wa CCM na wajumbe wa Kamati Kuu kunirudisha. Nimerudi katika Chama ambacho nimezaliwa na kukulia, Chama ambacho kimenisomesha,’’ alisema.
Aliongeza “Hivyo, niliahidi sitaondoka tena, nitabakia CCM hadi mwisho wa uhai wangu. Kurudi kwangu CCM nitaendelea kukitumikia Chama changu na sasa nitaendelea kushirikiana na Mbunge wangu Nape Nnauye. Mwaka 2015 nilisema nitawaletea Nape na kweli nilimleta, hivyo ya Mwaka 2015 nilisema nitawaletea Nape na kweli nilimleta, hivyo sasa Mtama mtakuwa na wabunge wawili, Mbunge wetu Nape na mimi mbunge wa chini chini,”alisema.
NAPE
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mtama ambaye ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema baada ya Membe kuondoka katika Chama wananchi wengi walichukia, lakini aliwaomba wasichukie kwani kuna siku moja atarejea.
“Leo (jana) mwenyezi Mungu ameturudishia faraja la Rondo, ameturejeshea furaha Chiponda. Mtama ni wastaarabu na hatuna shida tena,tuna imani kubwa na Membe, alinikabidhi kijiti na kuvaa viatu vyake, kulikuwa na mambo yaliyokwama huku nyuma kwa sababu za kisiasa, lakini Mama Samia amekuja ameziondoa,” alisema.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wa Mtama kushikamana, fitina ambazo ziliingia kati zimekwisha. “Membe amenipigania katika mambo mengi, nilipotaka ubunge Ubungo baada ya kuonekana fitina zimeingia katikati Membe aliamua kuchora ramani.
“Ndio maana safari yangu ya ubunge imekuwa nyepesi. Kaka Membe amenipigania sana na bahati nzuri amerudi CCM. Niseme tu Mungu ameamua ugomvi,” alisema.
SHAKA AMKABIDHI KADI
Akizungumza katika mkutano huo, Shaka alisema Membe amerejeshwa katika Chama baada ya kufuatwa kwa utaratibu ikiwemo kujadiliwa na tawi lake kisha na vikao vya juu.
Shaka alisema Membe na wanachama wengine zaidi ya 1670 waliovuliwa uanachama ambao wamejadiliwa katika vikao na kurejeshewa uanachama, sasa wanaweza kukabidhiwa kadi zao katika matawi yao.
Shaka alisema kurejea kwa Membe ndani ya CCM kuendelee kuwa chachu ya kudumisha umoja na mshikamano hususan kwa wanaCCM wa Jimbo la Mtama.
NA SOPHIA NYALUSI, Lindi