MAISHA ya miaka 41 katika sekta ya ujenzi yametosha kujenga historia iliyotukuka ya maisha ya duniani ya Mhandisi Patrick Mfugale.
Kile kinachoelezwa kuwa maisha yako ndiyo yatakayotafsiri kumbukumbu na alama za ulichokifanya ulimwenguni, kimeakisi uhalisia wa miaka 68 ya uhai wake.
Hata kama haukuwahi kusikia jina lake, bila shaka umepita katika moja ya miundombinu iliyojengwa kwa mchango wa taaluma na utendaji wake.
Huyu ni Mhandisi Patrick Mfugale, mwamba wa barabara na madaraja makubwa na madogo nchini, sifa hizo zinatokana na utumishi uliotukuka wa miaka 41 katika sekta ya ujenzi akishika nyadhifa mbalimbali.
Juni 14, mwaka huu, ilikuwa siku ya mwisho kuonekana hadharani akitekeleza majukumu yake, siku ambayo Rais Samia alifanya ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli, jijini Mwanza.
Juni 29, ndiyo siku aliyoumaliza mwendo, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, alikokimbizwa kupatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla wakati akitekeleza majukumu yake.
Mbali na alama alizoziacha jina lake litabaki milele, kutokana na moja ya miradi aliyoshiriki utekelezaji wake kupewa Jina lake nalo ni Daraja la Mfugale linalounganisha makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere.
Historia yake kazini
Mhandisi Mfugale alianza kazi Wizara ya ujenzi tangu mwaka 1977, ambapo hadi anafariki ameacha historia ya kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 36,258 na madaraja 1,400.
Baadhi ya waliowahi kufanyakazi naye, wanasema hakupenda kusifiwa katika utendaji wake, badala yake alishauri sifa hizo kuelekezwa kwa nchi yake.
Pia, Mhandisi Mfugale ndiye miongoni mwa wahandisi wachache walioamua kurejea nchini na kutumikia taifa baada ya kuhitimu taaluma hiyo, wakati wengi wao walitokomea nje ya nchi kufanya kazi huko.
Baadhi ya madaraja aliyosimamia na kusanifu ujenzi wake, yameingia katika orodha ya miradi 10 bora kwa urefu barani Afrika, likiwemo Daraja la JP Magufuli ambalo likikamilika litakuwa namba sita kwa urefu.
Hata hivyo Daraja la Benjamin Mkapa la Rufiji mkoani Pwani, limeingia kuwa namba tisa kwa urefu Afrika.
Pamoja na madaraja hayo mengine makubwa aliyosimamia ujenzi wake tangu alipokuwa Mhandisi wa madaraja na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ni Daraja laTanzanite, Kijazi Interchange na Mfugale Flyover.
Mhandisi Mfugale ndiye aliyebuni daraja la Malagarasi lenye urefu wa mita 178 kwa muda wa miezi mitatu na kuwa sehemu ya usanifu wa Daraja la Nyerere linalounganisha sehemu ya kati ya jiji na Kigamboni ambalo ni kwanza kujengwa baharini nchini lenye urefu wa mita 680 na upana wa mita 32.
Tangu alipoanza kazi kama fundi sanifu mwaka 1977 ufanisi wake ulimpandisha vyeo mbalimbali katika utumishi wake, ambapo aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa mwaka 1992.
Baadaye aliteuliwa kuwa Mhandisi Mkuu wa madaraja, mwaka 1992 na akiwa masomoni Uingereza mwaka 1995 alitafiti na kutengeneza mfumo wa usimamizi wa madaraja nchini.
Pamoja na kuanza kazi mapema, Mfugale alisajiliwa kama mhandisi mtaalamu mwaka 1991, mhandisi mshauri mwaka 2014 na pia ni mwanachama wa Chama cha Wahandisi Tanzania.
Kutokana na utendaji wake, Mhandisi Mfugale alitunukiwa tuzo mbalimbali ambapo mwaka 2003 alipokea tuzo ya mafanikio katika fani ya uhandisi na tuzo ya mhandisi bora mwaka 2018
Aidha, Mhandisi Mfugale amekua Mwenyekiti wa Kikosi cha Wataalamu cha Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ujenzi wa Dodoma Sports Complex na aliwahi kuwa mjumbe wa timu ya majadiliano ya mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge.
Wafanyakazi wenzake wamlilia
Hijja Malamla ni Mkurugenzi wa Fedha wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), aliyekuwa miongoni mwa wafanyakazi wenza wa Mhandisi Mfugale, anasema mbali na kuwa bosi lakini kiongozi huyo alisimama kama mzazi kwa wafanyakazi wenzake.
Anasema katika kipindi chote alichofanya kazi naye, alikuwa mithiri ya mzazi ambaye wakati wote alijikuta kushauri panapo kasoro.
Kwa mujibu wa Hijja, Mhandisi Mfugale katika uongozi wake TANROADS alipenda kutoa ujuzi na uzoefu wake hasa kwa wahandisi vijana.
“Alipenda ujuzi alionao uwafikie na wenzake, hakuwa mchoyo kimsingi alikuwa mlezi mzuri wa taaluma za vijana,” anasisitiza.
Hijja anaongeza kuwa Mhandisi Mfugale katika kipindi chote alichofanya kazi naye, hakuwahi kumuona akihamaki, badala yake alishauri na kusikiliza zaidi kisha kutoa maamuzi.
Anataja jambo lingine kumuhusu Mhandisi Mfugale ni kwamba hakuwa na haraka ya kufanya jambo ambalo aliona linahitaji utulivu.
Anamuelezea kuwa, alikuwa msikivu na hakudharau ushauri wa yeyote mwenye cheo na hadhi yoyote ofisini, bali akipenda kutoa changamoto kisha kutoa suluhu ya busara.
Anaeleza kuwa kiongozi huyo, alikuwa na maamuzi shirikishi kwani kila jambo bila kujali kubwa ama dogo aliishirikisha menejimenti kufanya maamuzi ya pamoja.
“Pamoja na yote Mzee Mfugale hakuwa na majivuno, hata ukimuona utadhani sio yeye mwenye jina kubwa linalofahamika na watu wengi,” anasema.
Anabainisha kuwa hata wakati watendaji wenye hadhi kama yake waliopatiwa walinzi binafsi, Mhandisi Mfugale alikataa hilo, kwa kile alichosema kuwa mlinzi wake ni Mungu pekee.
“Sikumuona akisema kwa hasira au jazba aliishia kushauri, huyu Mzee alikuwa na busara ya aina yake, hakika tumempoteza mtu makini,” anasema.
Anaeleza kuwa ukaribu wake na wafanyakazi haukuishia kazini pekee, bali hata aliwaalika mara kadhaa nyumbani kwake kwa shughuli za familia.
“Wema wake ulimfanya kuniunganisha familia ya TANROADS na familia yake, kama unavyofahamu wafanyakazi wengi inakuwa ngumu kupajua kwa mwenzako lakini Mzee wetu alitualika mara kwa mara,” Anaeleza.
Kuhusu mambo aliyochukizwa nayo, anayataja kuwa Mhandisi Mfugale, hakupenda uvivu, uzembe na kukosa udilifu katika kazi.
Anasema wakati wote alikuwa akiwaambia pengine kuna vitu vingi vinawashawishi TANROADS lakini ni vyema wafanye kazi kwa uadilifu, utendaji wao utaonekana tu.
Anafafanua kuwa pamoja na uzee wake lakini katika kazi iliyopangwa kumalizwa alikuwa tayari kutumia hata saa 24 ilimradi ikamilike, hivyo alikuwa mchapakazi mzuri.
Anaeleza kuwa, kiongozi huyo alipenda utani na watu wote, hilo aliahuhudiwa akilifanya mara kadhaa kwa watumishi wa ngazi mbalimbali wa TANROADS.
Wananchi
Hamza Kanali mkazi wa Dar es Salaam anasema alimtambua Mhandisi Mfugale baada ya uzinduzi wa Daraja la Mfugale Tazara jijini humo.
Anasema siku ya uzinduzi aliyekuwa Rais wakati huo alieleza sababu za kutoa jina hilo kwa Daraja lile, hivyo kupitia hilo alimfahamu.
Anafafanua kuwa kwa namna alivyoelezewa, anastahili kila aina ya heshima sio tu kwa utumishi wake, bali msaada alioutoa kwa wananchi kupitia maono yake.
Anaongeza pamoja na kwamba kila alilolifanya lilipata uwezeshaji kutoka serikalini lakini, taaluma yake amezitumia vyema kutekeleza wajibu wake na hatimaye imekuwa msaada kwa jamii.
“Siku hizi tunapita pale TAZARA bila msongamano kama ilivyokuwa awali, hata Ubungo pia, bila shaka kiongozi huyu ni miongoni mwa walioshiriki kufanikisha miradi hii,” anasema.
Changamoto
Akihutubia wananchi katika uzinduzi wa Barabara za juu za Mfugale aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dk. John Magufuli, alisema Mfugale amepitia changamoto nyingi katika utumishi wake ikiwamo kuamka nje ya nyumba aliyokuwa amelala na wakandarasi mkoani Ruvuma.
“Mfugale akiwa Songea kwa watani zangu wakiwa wamejenga kambi Matomondo na Kimesela, jioni yake walilala katika hako kajumba kesho yake waliamka saa nne wapo nje,” alisema.
Alieleza katika ujenzi wa barabara Matomondo fremu za greda ziliwahi kukatika wakati wa shughuli za utengenezaji wa barabara.
Aliongeza kazi hiyo iliendelea baada ya marehemu mzee Gama kuwaomba wanakijiji wa eneo hilo kuruhusu muendelezo wa utengenezwaji wa barabara hiyo kwa kuwa ilikuwa na manufaa kwao.
Hayati Dk. Magufuli alisema Mhandisi Mfugale amewahi kukaa ofisini bila kulala kwa siku tatu akibuni daraja la Umoja na kusahaulika katika utambulisho wa ufunguzi wa daraja hilo.
Hata hivyo, alimtaja kama mchapakazi, mzalendo, mbunifu na mwaminifu katika kazi zake na kwamba hakupendelewa kwa uamuzi wa flyover hiyo kupewa jina lake.
“Kwa naamna ya pekee nimpongeze mtendaji mkuu wa Tanroad Mhandisi Patric Mfugale kwa kusiriki kubuni nakusimamia michoro katika kutelekeza mradio huu,” alisema.
Maisha yake
Mhandisi Mfugale alizaliwa Desemba mosi, mwaka 1953, Ifunda mkoani Iringa na alianza elimu ya msingi mkoani humo.
Elimu yake ya Sekondari alihitimu mwaka 1975 katika Shule ya Sekondari Moshi.
Mwaka 1983, alihitimu Shahada ya kwanza ya uhandisi kutoka Chuo Kikuu cha Rokii India na shahada ya pili kutoka Chuo Kikuu cha Loughborough Uingereza mwaka 1995
Mwili wa Mhandisi Mfugale utasafirishwa kesho jioni kwenda Ifunda mkoani Iringa, kwa ajili ya maziko yatakayofanyika jumatatu.
Na JUMA ISSIHAKA