POLISI Mkoa wa Manyara, inamshikilia mfanyakazi wa ndani, Januari Makomolwa, mkazi wa Kijiji cha Endagikok, wilayani Mbulu, kwa tuhuma za kumnajisi mwanafunzi wa darasa la kwanza mwenye umri wa miaka saba.
Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Manyara, Marrison Mwakyoma, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 18 mwaka huu, ambapo mtuhumiwa alimbaka mtoto huyo (jina limehifadhiwa).
Alieleza kuwa Makomolwa aliyekuwa akifanya kazi katika familia ya mtoto huyo inadaiwa aliachiwa mtoto na bosi wake, ndipo alipoamua kufanya kitendo hicho.
Mwakyoma alisema matukio ya ubakaji yamekuwa yakiongozeka katika mkoa huo, hivyo aliwataka wananchi wanapoajiri wafanyakazi wa ndani, wahakikishe wanawachunguza tabia zao kwanza.
“Tusiwaamini wafanyakazi wa ndani kwa kuwa ndugu wa karibu na marafiki wa familia ndiyo wanabaka watoto,” alisema.
Katika tukio lingine, polisi inamshikilia mkazi wa Kijiji cha Bassoutu, Elibariki Shaban, kwa tuhuma za kumpiga mtoto wake, Amos Elibariki (25) hadi kufariki dunia.
Kamanda Mwakyoma alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 26, mwaka huu, saa 3:00 za usiku.
Alisema mtuhumiwa alipohojiwa na polisi sababu za kumpiga mwanae alidai alimpiga kwa kuwa mtoto huyo alimtukana, hivyo hasira zilimpanda na kuamua kumwadhibu kwa kumpiga na deki, mateke na makofi.
Kamanda huyo wa polisi alisema Amos alifariki dunia wakati wakipelekwa katika hospitali ya Hydom kwa matibabu.
Wakati huo huo, mtoto wa miaka (10) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Walleta iliyopo Wilaya ya Hanan’g, amekutwa amefariki dunia katika ghala la kuhifadhia mazao.
Kamanda Mwakyoma alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 23, mwaka huu, saa 2:30 asubuhi katika wilaya hiyo.
Alisema wananchi walibaini mtoto huyo amefariki dunia baada ya kumtafuta bila mafanikio na baadaye walikuta shati lake likining’inia dirishani kwenye ghala la Elizabeth Ama.
Mwakyoma alisema wananchi baada ya kugundua mtoto huyo yupo kwenye ghala hilo walimtafuta mmiliki wa ghala ambapo walimkuta ameangukiwa na magunia ya mahindi huku mkononi akiwa ameshikilia kisu ambacho alikuwa anakitumia kuchana magunia.



























