MGOMBEA Uenyekiti wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), Shendu Mwagalla, amesema kama akiibuka kidedea katika uchaguzi ujao, moja ya vipaumbele vyake ni kuboresha mashindano ya timu za watu wenye ulemavu kuwa na viwango vya juu.
Uchaguzi wa BD unatarajiwa kufanyika Julai 10, mwaka huu, ili kupata viongozi wapya ili kuendeleza na kukuza mchezo wa kikapu Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza na Uhuru Digital, Mwagalla amesema endapo atapata nafasi ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti, atahakikisha timu za wachezaji wenye ulemavu wanapata nafasi ya kushiriki mashindano ya mara kwa mara.
Mwagalla amesisitiza kuwa wachezaji hao wanafanya mazoezi muda mrefu bila kupata mashindano ya kupima viwango vyao, kitendo kinachosababisha kutokuwa na timu ya Taifa yenye uwezo mzuri.
“Kama nikipata nafasi ya kuchaguliwa kuongoza kama Mwenyekiti, nitahakikisha ninasimamia vyema michuano ya watu wenye ulemavu ili kupata timu nzuri ya Taifa itakayokuwa ikituwakilisha katika mashindano mbalimbali.
“Pia nitatengeneza mikakati ya kuendesha mashindano ya kitaifa ya kila mara tofauti na ilivyokuwa awali,” amesema.
Na AMINA KASHEBA