TAARIFA iliyotufikia punde, imeeleza kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, amefariki dunia.
Chanzo cha kuaminika kimeiambia Uhuru Digital, kuwa Mzee Mfugale amefariki dunia ghafla leo, katika hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma, baada ya kuzidiwa akiwa kikaoni.
Majina yake kamili ni Patrick Aron Mfugale, alizaliwa Ifunda, Mkoani Iringa.
Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Consalata Fathers Primary School mjini
Iringa; Mwaka 1975 alihitimu elimu yake ya shule ya upili katika shule ya upili ya Moshi.
1977, aliajiriwa katika Wizara ya Ujenzi
1983, alitunukiwa Shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Rocky nchini India.
Mwaka 1991, Mfugale alisajiliwa kama Mhandisi mtaalam na baadaye mwaka 1992, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa barabara za mikoa.
1994-1995- Alitunukiwa Shahada yake ya pili katika Chuo kikuu cha Loughborough, Braunshweig nchini Uingereza.
2003- Alipokea tuzo ya Distinguished Engineering Accomplishment na kuteuliwa kuwa Mhandisi Mkuu wa madaraja hapa nchini Tanzania.
Akiwa masomoni nchini Uingereza mwaka 1995, alitafiti na kutengeneza mfumo wa madaraja nchini na mfumo wa usimamizi wa madaraja kwa jina Tanzania Bridge Management System.
2014- Alisajiliwa kuwa mhandisi mshauri na kuwa mwanachama wa Chama cha Wahandisi Tanzania.
Ametumia muda wake mwingi kama mtaalamu wa madaraja, ambapo alibuni daraja la Malagasi lenye urefu wa mita 178 na kujengwa kwa sh.milioni 300.
Baadhi ya madaraja aliosimamia ujenzi wake ni:
-Daraja la Mkapa, Rufiji
-Daraja la Umoja linalounganisha Tanzania na Msumbiji, Ruvuma.
-Daraja la Rusumo, huko Mara
-Daraja la Kikwete huko Malagasi
-Daraja la Nyerere huko Kigamboni
Mfugale ambaye hadi umauti unamkuta alikuwa mtendaji mkuu wa TANROADS, amesaidia kufanikisha ujenzi wa madaraja 1,400 hapa nchini.
Amebuni na kusimamia barabara za kitaifa zenye urefu wa takriban kilomita 36, 258.
Alikuwa Mwenyekiti wa kikosi cha ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR), inayoendelea kujengwa.
Alikuwa mjumbe wa timu ya majadiliano ya miradi mikubwa ya umeme nchini.



























