Na INNOCENT BYARUGABA, Kibaha
SERIKALI ya Awamu ya tano inaamini kuwa kila mwananchi anapaswa kujishughulisha kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kujiletea maendeleo yake na taifa kwa ujumla. Imani hii ndiyo chimbuko la kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Kwa upande wake inatambua kuwa inalo jukumu la kuhakikisha kuwa walio wanyonge katika jamii wanapata fursa ya kustawisha maisha yao na kuondokana na unyonge wao ili kupunguza tofauti za matabaka ya kichumi. Yaani mwenye nacho na asiyekuwa nacho! Kila mmoja afanye kazi. Hata maandiko matakatifu yanasisitiza kufanya kazi. ‘Na asiyefanya kazi asile’.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, amejiwekea utaratibu wa kufanya ziara mara kwa mara kwenye maeneo ya uzalishaji mali, ujenzi wa miundombinu na maeneo ya wafanyabiashara wadogowadogo, kuona shughuli wanazofanya, kusikiliza kero zinazowakabili na kuzitatua
Kero za kubomolewa kwa soko la Picha ya Ndege, lililopo kandokando ya barabara ya Morogoro mwanzoni mwa mwezi Februari, 2021 na changamoto za miundombinu katika soko la Mnarani, zilimpeleka Mhandisi Ndikilo na Kamati ya Ulinzi na Usalama kujionea hali halisi na kufanya mikutano ya hadhara na wafanyabiashara kwenye masoko hayo, yaliyopo kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha, akianza na Soko la Picha ya Ndege kisha Loliondo.
Ziara hiyo pia iliwajumuisha wataalamu kutoka taasisi nyingine ikiwamo Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Barabara (TANROAD), Wakala wa Usafiri Nchikavu (LATRA) na Shirika la Majisafi na Majitaka (DAWASA) kwa ajili ya kutoa majawabu kwa wafanyabiashara.
Akiwasilisha kero zinazowakabili wafanyabishara wa soko jipya lililoongeza idadi ya wafanyabiashara kutoka 150 hadi 520, Diwani wa Kata ya Sofu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Mussa Ndomba, aliitaja moja ya changamoto zinazowakabili ni umeme na maji ambapo anaziomba mamlaka husika hufikisha huduma hizo zitakazowawezesha wafanyabiashara kuzipata kwa gharama nafuu.
Pia, Ndomba anaomba kujengwa kwa kituo kipya cha daladala kitakachoshusha na kupakia abiria katika eneo hilo na kuimarishwa kwa kalvati linaloruhusu magari ya mizigo kuingia kutokana na kuongezeka kwa magari yaliyochepushwa njia kupisha utanuzi wa barabara eneo la Picha ya Ndege.
Mbali na hilo, alisema changamoto nyingine ni kuondolewa kwa wafanyabiashara waliobakia soko la zamani kwani mazingira yake sio rafiki kwa afya na usalama wa binadamu kutokana na vumbi, mitambo iliyoegeshwa na maligahafi za ujenzi unaoendelea.
Ndomba aliomba baraka kwa mkuu wa Mkoa kuanzishwa kwa mnada wa gulio na mbuzi nyama choma, kuchangamsha soko na kuwahamasisha wanunuzi kufika kufanya ununuzi ili kuongeza mapato ya halmashauri.
“Mheshimiwa mkuu wa mkoa natamani sana soko hili lisimame, wajasiliamali ili hawa wadogo wapate mikopo kutoka halmashauri na taasisi nyingine za kifedha wafanye biashara zenye tija. Sisi tunataka maendeleo….Tuachane na siasa kwani kipindi cha kampeni kimepita sasa ni utekelezaji,” anasema Ndomba.
Mhandisi Ndikilo akizungumza na wafanyabiashara hao, anakiri kupokea malalamiko ya wafanyabiashara kuondolewa kwenye eneo la Picha ya Ndege na kupelekwa mahali ambapo wanadai hakuna miundombinu ilhali wakiwa na vitambulisho vya wajasiriamali, huku wakiwa na mikopo kutoka taasisi za kifedha zikiwamo benki hali ambayo itawafanya washindwe kulipa mikopo hiyo.
Anasema sababu za wafanyabiashara kuondolewa eneo hilo lenye upana usiozidi mita 20, ni ufinyu wa eneo lenyewe, vumbi jingi linalotokana na shughuli za ujenzi unaoendelea na mitambo iliyoegeshwa, msongamano mkubwa wa watu pamoja na bodaboda, biashara ya ukaangaji wa chipsi hali inayoweza kusababisha kulipuka kwa magari yanayobeba matenki ya mafuta.
“Fedha zinatafutwa ndugu zangu, lakini roho ya mtu haipatikani popote ikishatoka ndio basi tena. Awe mjomba, bibi, mama akishaondoka ameondoka. Nawapenda sana wananchi wangu, binafsi pamoja na kamati yangu ya ulinzi na usalama hatupo tayari kuona mkipata madhara ambayo yanaonekana. Nayasema haya kwa nia njema kabisa ya kuokoa maisha yenu,” anasema.
Ndikilo anakiri kuwa barabara kuu ya Morogoro ndio uchumi wa nchi. Inapofungwa kwa sababu za ajali au vurugu za wafanyabiashra wanaofanya biashara zao kwenye ‘road reserve’ (hifadhi ya barabara), inasitisha shughuli nyingine kuendelea ikiwamo bandari, kwani zaidi ya asilimia 80 ya makontena yanayoshushwa yanategemea barabara ya Morogoro ambayo ni kiunganishi cha mataifa ya Kaskazini na Kusini mwa Tanzania, “maana yake tutapoteza diplomasia ya uchumi kwa nchi jirani.”
Ndikilo anatumia jukwaa hilo kuwaonya wenye maduka lilipokuwepo soko la Picha ya Ndege kuacha kujaribu kupimana ubavu na serikali kwa kuwahamasisha wafanyabiashara kutokubali kuhama kwa maslahi yao binafsi.
Anasema inajulikana kuwa baadhi ya wenye maduka ambao walikua wakiwalipa wafanyabiashara waliokuwa wakipanga bidhaa mbele ya maduka yao, pia anawataka wanasiasa uchwara kujiepusha na uchochezi unaolenga kuharibu mipango mizuri ya serikali.
KAULI ZA WAJASIRIAMALI
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Ndikilo, Rukia Saidi na Mwanahamisi Ramadhani wajasiriamali wanaojishughulisha na uuzaji wa mbogamboga sokoni hapo, wanaomba kujengewa banda maalumu kwa ajili ya biashara zao litakalowakinga dhidi ya mvua na jua.
“Bado tunakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na banda la kutukinga dhidi ya mvua na jua, tunaiomba serikali iliangalie hili na kulipatia ufumbuzi ili kujengea mazingira mazuri ya ufanyaji wa shughuli zetu.
Saidi Utipula na Mohamedi Unembwe ambao pia wafanyabiashara katika soko hilo, wanaomba halmashauri kushusha kodi ya wauzaji wa matunda kutoka sh. 10,000 inayolipwa sasa hadi 5000 huku kodi ya fremu za maduka wakiomba zishushwe kutoka sh. 8,000 hadi 3,000.
Kwa upande wake, Diwani wa Tangini, Mfalme Kabuga anaiomba serikali kutazama kuharibika kwa miundombinu ya barabara ambayo imekuwa ikisababisha changamoto kubwa hususan wakati wa mvua ambapo husababisha magari yanayoleta bidhaa sokoni hapo kushindwa kufika na kuwalazimu wafanyabiashara kuingia gharama ya ziada ili kuzifikisha.
MAAGIZO YA RC NDIKILO
Katika kutatua changamoto hizo, Mhandisi Ndikilo alitoa maagizo kadhaa yanayolenga kufanikisha ufanyikaji wa biashara kwa ufanisi zaidi sokoni hapo.
Mosi, watendaji wa halmashauri wakamilishe miundombinu wezeshe yote ikiwamo choo, umeme na maji ili soko lianze kufanyakazi.
Aidha, alizitaka taasisi hizo kufanya tathmini ya kutosha na kuwasilisha gharama nafuu ambazo wafanyabiashara wadogo watamudu kuzilipia.
Pili, aliiagiza TANROAD kuendelea kuihudumia barabara inayojengwa kwa kuimwagia maji ili kupunguza vumbi huku akiiagiza TARURA kuweka makalvati kwenye sehemu zote yanakohitajika na kuhakikisha barabara zote zinafanyiwa matengenezo ili kupitika muda wote.
Aidha, aliiagiza LATRA kujenga kituo cha daladala kitakachotumika kupandisha na kushusha abiria aneo la soko.
Tatu, aliagiza ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri kuratibu uanzishwaji wa mnada wa gulio na mbuzi nyama choma utakaokua unafanyika kila Alhamisi, ili kuhamasisha wanunuzi wa bidhaa kwenye soko hilo la Msufini.
Nne, halmashauri inaekelezwa kujenga banda la wauza matunda na mbogamboga litakalowakinga na mvua, jua huku wakikaa meza moja na wafanyabiashara kuangalia namna ya kupunguza ushuru kutoka sh. 10,000 unaolipwa sasa hadi sh. 5,000 kama inafaa
Tano, wataalamu wa halmashauri kufanya ukaratabati kwenye mabanda yanayovuja kujadiliana na wafanyabiashara namna ya kupungaza kodi hadi sh. 3,000 kutoka sh. 8,000 inayolipwa sasa kama sheria mama na sheria ndogo zinaruhusu
Sita, anamwagiza Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani kuhakikisha magari yanayobeba abiria yanapita sokoni hapo, kuingia stendi na sio kukatisha njia au kushusha abiria nje ya stendi hata kama basi litakua na abiria mmoja kwa kuwa hiyo ndio sheria.
Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi ya 2020-2025, inaielekza serikali kuhamasisha na kusimamia halmashauri zote nchini kuendelea kutenga, kurasimisha na kupima na kuweka miundombinu kwenye maeneo maalumu kwa ajili ya uwekezaji na kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kujishughulisha na uzalishajimali na biashara.
Serikali chini ya Rais Magufuli imeendelea kuimarisha mifumo ya kisera, kitaasisi na kisheria, ikiwamo kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambapo kwa robo ya kwanza Julai–Oktoba, halmashauri ya Mji Kibaha imeshatoa zaidi ya sh. milioni 243, kwa makundi hayo ili kuyajgea uwezo wa kiuchumi.