Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Wakili Stephene Byabato (Mb) amefanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Irani nchini Mhe. Hossein Alvandi Bahineh katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo yao yalijikita kujadili masuala mbalimbali ya kukuza na kudumisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya kimkakati ikiwemo biashara na uwekezaji, kilimo, nishati, ulinzi na usalama.
Katika mazungumzo hayo Waziri Byabato amemweleza Balozi wa Iran Mhe. Bahineh kuhusu nia na utayari wa Tanzania katika kuendeleza ushirikiano kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi na Iran sambamba na kuendelea kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano kwa maslahi ya pande zote mbili.
Kwa upande wake Balozi wa Iran Mhe. Bahineh ameeleza kuwa nchi yake inauzoefu wa muda mrefu wa kuendesha miradi mikubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati, hivyo kwa kutumia uhusiano mzuri uliopo kati ya mataifa hayo Tanzania ina fursa ya kipekee ya kunufaika na utaalamu na ujuzi ambao utaweza kuchagiza maendeleo ya sekta ya nishati nchini.