WATANZANIA wanaadhimisha miaka 60 ya Uhuru mwaka huu ambao Tanzania imeandika historia ya kuwa na Rais mwanamke Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wa kuongoza nchi kwa umahiri na kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano.
Rais Samia ambaye anatarajiwa kuwaongoza Watanzania, katika maadhimisho ya aina yake ya miaka 60 ya Uhuru wa nchi yetu, aliingia madarakani Machi 19, mwaka huu baada aliyekuwa Rais wa awamu ya tano , Dk. John Pombe Magufuli, kufariki dunia Machi 17.
Akiwa Makamu wa Rais, Samia aliapishwa kushika wadhifa huo wa Rais, katika hali ya changamoto za msiba mzito wa kumpoteza mkuu wa nchi, lakini alionyesha uwezo wa hali ya juu, aliwaongoza Watanzania katika hatua mbalimbali hadi maziko yaliyofanyika Chato mkoani Geita.
Katika kipindi kifupi cha uongozi wake, Rais Samia, amefanya mambo mengi makubwa, ikiwemo kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji, kwa kuboresha baadhi ya mifumo na kufungua fursa zaidi kwa wawekezaji kuja kuwekeza nchini.
MIRADI YA TRILIONI 8
Takwimu zinaonyesha, kumekuwa na ongezeko kubwa la usajili wa miradi ya uwekezaji yenye thamani ya sh. trilioni nane na inatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja 38,000.
Ongezeko la usajili wa miradi hiyo, ni matokeo ya maboresho ya mifumo na kuongolewa kwa changamoto mbalimbali zilizowakatisha tamaa wawekezaji waliokuwa wanakuja kuwekeza nchini.
Katika kipindi hicho takwimu za wizara ya uwekezaji, zinaonyesha ongezeko hilo ni sawa na asilimia 500, jambo ambalo halijawahi kutokea katika awamu zingine za uongozi, jambo linalomweka Rais na serikali katika viwango vya juu.
Takwimu za mwaka jana katika kipindi kama hicho, zinaonyesha usajili wa miradi ulikuwa wa thamani ya Dola za Marekani milioni 647.43.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Godfrey Mwambe, akizungumza hivi karibuni kuhusu mafanikio ya miaka 60 Uhuru, katika wizara hiyo, alitaja maeneo mbalimbali ambayo wamefanya vizuri zaidi tofauti na mwaka jana.
Mwambe anaeleza kwamba, kwa kipindi cha awamu hii miradi ya TIC itatoa ajira 32,715 ikilinganishwa na ajira 10,000 kwa kipindi kama hicho mwaka jana. Hii ni kutokana na agizo la Rais Samia ya uandaaji wa mabenki ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na TIC wamekamilisha kazi ya kubainisha maeneo ya uwekezaji yaliyotengwa.
Mpaka sasa anasema wameanzisha kanzidata yenye jumla ya hekta 1,606,193.40 za ardhi, ambapo TIC sasa wanajenga mfumo wa kuhifadhi taarifa za upatikanaji wa ardhi kwa wawekezaji.
Mwambe anasema mfumo wa mtandao wa Portal utakuwa msaada mkubwa kwa wawekezaji kufahamu maeneo yanayofaa na yanayopatikana kwa uwekezaji kwa njia ya mtandao, huku akieleza kuwa ardhi iliyotengwa kwa kilimo biashara, makazi, viwanda, hoteli, hospitali, shule za sekondari, zitapunguza usumbufu wa upatikanaji wa vibali vya kazi.
“Tunatekeleza maagizo ya Rais Samia ya kuondoa urasimu katika upatikanaji wa vibali vya kazi, ndani ya siku moja mwombaji hupatiwa kibali kupitia mfumo wa ki elektriniki ,’’anaeleza.
Anasema kupitia dawati waliloanzisha la kupokea malalamiko ya uwekezaji,ofisi yake ilipokea changamoto 112 kutoka kampuni 92, ambapo kati ya hizo tayari 19 zimepatiwa ufumbuzi na zingine zinaendelea kutafutiwa majawabu.
Mwambe anabainisha kuwa serikali inaendelea kuboresha mazingira kwa wawekezaji ili kusaidia sekta binafsi kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa taifa na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Anaeleza kuwa, serikali itaimarisha miundombinu ya barabara, reli, madaraja, umeme, viwanja vya ndege lengo kupunguza gharama za uzalishaji ikiwa na kutengwa kwa maeneo ya biashara na kuongeza ushiriki wa watanzania katika miradi ya kimkakati na kuboresha utoaji wa mikopo kwa kupunguza riba na masharti mengine.
Mwambe anasema, atahakikisha wazawa wanapata fursa ya kushiriki katika miradi ya kimkakati na miradi ya uwekezaji .
Kwa upande wa mitaji Mwambe anasema, wizara imeweka mazingira ya upatikanaji wa mitaji kwa kuimarisha vyanzo vya mikopo ili kuwanufaisha wananchi ambapo wameanzisha mifuko na programu 52, mifuko 21 hutoa mikopo moja kwa moja, dhamana, mifuko 17 hutoa ruzuku na programu tano za uwezeshaji.
Anaeleza kuwa mifuko ya uwezeshaji inayotoa mikopo na dhamana imetoa mikopo ya sh.trilioni 4.97 kwa wajasiriamali 7,231,617 wakiwemo wanawake 3,795,598 sawa na asilimia 52.5 na wanaume 3,436,019 sawa na asilimia 47.5,
“Mifuko imetengeneza ajira 13,591,146 ambapo kati ya hizo, ajira 8,018,775 sawa na asilimia 59 ni za moja kwa moja na ajira 5,572,371 sawa na asilimia 41 sai za moja kwa moja,’’anasema.
Mwambe anawataka wananchi kuanzisha shughuli za kiuchumi na kuendeleza vikundi vya kifedha vya kijamii.
“June, mwaka huu vikundi 30,484 vimeanzishwa vyenye wanachama 914,520 ambapo kati ya wanachama waliopo katika miavuli, wanawake 731,616 na wanaume 182,904, jumla ya mitaji iliyokusanywa kupitia miamvuli hiyo ni sh. trilioni 1.7,’’anaeleza.
Waziri huyo anasema katika kuimarisha na kukuza ushirika nchini hadi Juni, mwaka huu kuna vyama vya ushirika 9,185 vyenye jumla ya wanachama 6,050,324, ambapo wanaume 3,932,711 na wanawake 2,117,613.
Anaeleza kuwa kati ya vyama, Vyama vya Ushirika wa Masoko ya Mazao (AMCOS) vilikuwa 4,039 vyenye wanachama 2,660,562, Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) 3,831 vyenye wanachama 2,523,548.
Pia Vyama vya Msingi (Union) vilikuwa 58 vyenye wanachama 38,206, Vyama vya Joint enterprises vilikuwa 42 na wanachama 27,666 na Vyama vingine vilikuwa 1,215 na wanachama 800,342,.
UWEZESHAJI
Mwambe anasema, wizara ilianzisha vituo vya uwezeshaji 17 katika Mikoa ya Singida (1), Shinyanga (1) Kigoma (6), Dodoma (7), Rukwa (1) na Geita (1) kama iliyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025 katika Ibara ya 26 (K).
Anasema vituo vinavyotoa uwezesaji kwa wananchi na uendelezaji wa biashara na mikopo ni 10,893 wakiwemo wanawake 5,781 sawa na asilimia 53 na wanaume 5,112 sawa na asilimia 47.
Anaeleza kuwa vituo hivyo vimetoa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 44.5 kwa wananchi 4,474 ambapo wanawake 1,903 na wanaume 2,571.
Vilevile, vituo vimewezesha urasimishaji wa biashara 5,721 na kutoa mafunzo ya ujuzi na ujasiriamali kwa wananchi 6,339 wakiwemo wanawake 4,16 na wanaume 2,113;
Mwambe anaeleza, kuwa serikali imeendelea kutenga maeneo wezeshi ya kufanyia biashara kwa kundi la wanawake na kuwawezesha kufanya kwa ubora na kwa kiwango cha kitaifa na kimataifa.
MABORESHO YA SERA
Mwambe anasema, serikali imeweka mazingira wezeshi kwa watanzania kushiriki katika miradi ya kimkakati na kufanya mapitio ya sera na marekebisho ya sheria .
Anabainisha kuwa sera na sheria zenye kuhusisha ushiriki wa watanzania ni Sera ya Nishati, 2015, Sheria ya Mafuta, 2015, Kanuni za Ushiriki wa Watanzania katika sekta ya mafuta 2017, sheria ya madini, 2010 (kama ilivyorekebishwa mwaka 2017), .
Pia anataja kanuni za ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini, 2018, sheria ya bima 2009 na Kanuni zake, kanuni ya huduma ndogo za fedha 2019, sheria ya ununuzi wa umma, 2011 na sheria ya Wakala wa Meli Tanzania, 2017.
“Miradi mingi kwa sasa, ajira za ujuzi wa kati na zisizohitaji ujuzi kwa zaidi ya asilimia 90 zinafanywa na watanzania na wageni wameajiriwa zaidi katika ajira za ujuzi wa juu.
Wafanyakazi wa kitanzania 18,000 sawa na asilimia 82 ya wafanyakazi wote wameajiriwa katika ujenzi wa reli ya mwendokasi 3,487 sawa na asilimia 91 wameajiriwa katika uboreshaji wa reli ya kati.
‘’Mradi wa uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere umeajiri watanzania 997 sawa na asilimia 95 ya wafanyakazi wote. Barabara ya juu ya ubungo imeajiri Watanzania 1,845 sawa na asilimia 95 ya wafanyakazi wote, mradi wa matengenezo ya daraja la selander umeajiri watanzania 405 sawa na asilimia 91 ya wafanyakazi wote,’’anaeleza.
Pia, mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere umeajiri watanzania 4,783 sawa na asilimia 88 ya wafanyakazi wote,’’anaeleza.
Mwambe anasema serikali imekuza ajira katika migodi, ambapo watanzania wameendelea kupewa kipaumbele kutokana na maboresho katika sekta ya madini ikiwemo marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2010.
Anaeleza kuwa serikali imechukua hatua za kukuza uchumi na kuboresha hali ya maisha ya wananchi kwa kuhamasisha uwekezaji na ushiriki wa wananchi katika uchumi.
Mafanikio yaliyopatikana ni kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, utoaji wa mikopo kwa wajasiliamali, ujenzi wa miundombinu umeme, reli, barabara, madaraja, utoaji wa elimu kwa wajasiriamali, utoaji wa huduma za kijamii afya, elimu, na ujenzi wa vituo vya uwezeshaji,’’anasema..
Mwambe anasema serikali inaendelea kuchukua hatua za kusimamia na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo sheria, Kanuni na maelekezo ya uwekezaji kuhakikisha vikwazo vinatambulika na kuondolewa na kuwa na mazingira rafiki na sawa katika uwekezaji,”anasema .
Rais Samia mapema baada ya kuingia madarakani, aliagiza uongozi wa wizara ya uwekezaji ijipange ,ifanye kazi na akatoa miezi sita ili watendaji wake wafanye maboresho mbalimbali na kuhakikisha wanafanya kazi bila kukwamisha wageni wanaokuja kuwekeza nchini.
Msisitizo wa Rais Samia ni kuona wizara hiyo inaunganisha shughuli zake katika mfumo mmoja, ikiwemo utoaji wa vibali vya kazi na masuala ya ardhi kwa wekezaji, wasizungushwe bali waunganishwe ili mahitaji yao yafanyiwe kazi kwa haraka katika kipindi kifupi.
SELINA WILSON NA BARAKA LOSHILAA