RAIA wa Kenya ambaye alikuwa dereva wa Lori lenye namba za usajili KAS 924 U, Carlos Mahucha Otieno (43) amehukumiwa kwenda jela miaka 20, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha magunia 89 ya bangi yenye uzito wa kilo 2,830.2.
Akisomewa hukumu hiyo katika kesi ya jinai namba 71/2021, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Frank Mahimbali, alisema mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka bila kuacha shaka.
“Kutokana na ushahidi uliotolewa upande wa mashitaka kwa mashahidi saba na vielelezo tisa katika mahakama hii bila kuacha shaka, mahakama imeunga mkono ushahidi huo na kumuhukumu Carlos Otieno kwenda jela miaka 20.
“Kwa muda aliokaa gerezani takribani miaka sita, atapunguziwa adhabu na magereza kutumikia miaka 14 ukiondoa hiyo aliyokaa gerezani na kama hakuridhika siku 30 anaweza kukata rufaa,” alisema Jaji Mahimbali.
Awali, Mwanasheria wa Serikali, Mafuru Moses, alidai mtuhumiwa
Otieno mnamo Mei 25 mwaka 2016, alfajili saa 12 alikutwa na
Polisi wa Kituo cha Sirari waliokuwa doria katika kijiji cha
Kitagasembe, Kata ya Gwitiryo, Tarafa ya Inchugu, wilayani Tarime.
Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akiendesha lori aina ya Fuso lenye namba za usajili KAS 924 U na walipomsimamisha alipohojiwa alisita kuwajibu askari polisi na kusababisha polisi kumtia mashaka.
“Walipotia shaka mzigo uliobebwa ndani ya lori hilo walimuamuru kuendesha lori hilo hadi kituo cha Polisi Sirari huku wakiongozana. Lori lilipofika kituo cha Polisi waliita mashuhuda wakati wanafungua lori hilo ambapo walipofungua walikuta magunia 89 ya bangi yenye
uzito wa kilo 2,830,” alieleza.
Akijitetea mshitakiwa huyo kabla ya hukumu, alijitetea akidai kuwa sio dereva na hajui kuendesha na siku ya tukio alitoka kwake Migori nchini Kenya kuja Sirari kununua mchele kwa matumizi lakini alipofika Sirari mpakani alikamatwa na askari Polisi na kufunguliwa kesi ya kusafirisha bangi.
Mshitakiwa huyo aliiomba mahakama kumwachia huru kwani amekaa gerezani miaka sita na ana mke na watoto wawili wanaomtegemea.
NA SAMSON CHACHA, TARIME



























