Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Deogratius Ndejembi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Isaya Mbenje na watendaji walio chini yake kujitafakari juu ya mwenendo wa utendaji kazi wao kutokana na kushindwa kusimamia miradi inayotekelezwa kwenye halmashauri hiyo.
Ndejembi ametoa kauli hiyo alipotembelea miradi ya elimu ya msingi na sekondari inayotekelezwa kwenye halmashauri hiyo ikiwa ni maandalizi ya kupokea wanafunzi wa mwaka mpya wa masomo 2024.
Katika ziara yake, Naibu Waziri Ndejembi ameonesha kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Pangani Halisi iliyogharimu kiasi cha Sh bilioni moja, Shule ya Sekondari Masiaka inayojengwa kupitia mradi wa SEQUIP inayogharimu Sh milioni 585 na Shule ya Msingi Bushiri iliyogharimu Sh milioni 440 ikijengwa kupitia mradi wa BOOST.