MAZINGIRA mazuri ya uwekezaji nchini yamemuwezesha mfanyabiashara maarufu bilionea, Mohammed Dewji ‘Mo’, kutunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu wa udaktari ya mchango wa kusaidia jamii na hisani.
Mo ambaye ni rais wa Kampuni ya Mohammed Enterprise (MeTL) na mwanzilishi wa Mo Dewji Foundation, ametunukiwa shahada hiyo na Chuo Kikuu cha Georgetown, Shule ya Biashara ya McDonough, kilichopo Washington D.C. Marekani, jana.
Shahada hiyo ya uzamivu ya heshima ilitolewa na rais wa chuo hicho, John DeGioia, akisema wametambua mchango mkubwa wa Mo Dewji kwa jamii kupitia kazi zake za hisani nchini Tanzania.
Dewji alihitimu kutoka chuo hicho Kikuu cha Georgetown Shule ya Biashara ya McDonough, mwaka 1984, kabla ya kuzindua biashara zake akiwa ni rais wa MeTL Group na Mwanzilishi wa Mo Dewji Foundation.
Shahada hiyo ya udaktari inayotambua mchango wa kibinadamu na hisani ni ya heshima inayotolewa kwa waliojitofautisha kupitia michango wao kwa jamii.
Mo kupitia Mo Dewji Foundation imekuwa ikisaidia jamii, kutoa ufadhili wa masomo ya udaktari kwa baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kwa kushirikiana na serikali.
Pia kupitia kampuni zake za MeTL imekuwa ikichangia ajira na kulipa kodi serikalini.





























