MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango, ameuagiza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Jiji la Dodoma na ofisi ya mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais, kuhakikisha wanalinda bustani za miti zilizoanzishwa Dodoma na kuhamasisha wananchi kupanda miti ili kukabiliana na ukame katika jiji hilo.
Alitoa agizo hilo alipotembelea na kukagua bustani za miti zilizoko eneo la Medeli jijini Dodoma zinazomilikiwa na TFS na bustani inayomilikiwa na Jiji hilo.
Dk. Mpango aliiagiza Mamlaka ya Jiji hilo, kusimamia taasisi za serikali, binafsi na wafanyabiashara walioko kandokando mwa barabara kuhakikisha wanapanda miti na kuisimamia ili kupendezesha jiji la Dodoma na kukabiliana na ukame.
Aidha, aliwataka wataalamu kutoka idara ya mazingira kuacha kukaa ofisi, badala yake kwenda kwa wananchi kuwasaidia katika upandaji miti.
Pia, aliitaka TFS kutoa elimu ya miti kwa wananchi mara kwa mara ili kuwaepusha kupanda miti inayoweza kuharibu vyanzo vya maji na majengo.

Makamu wa Rais huyo, aliuagiza uongozi wa jiji la Dodoma kutumia sheria zilizopo kukabiliana na waharibifu wa mazingira ikiwemo uchomaji moto maeneo yaliyopandwa miti.
Dk. Mpango aliagiza katika upangaji wa miji kuhakikisha kunazingatia maeneo ya kilimo na bustani za miti ili kutopoteza maeneo yote katika ujenzi wa majengo na baadaye kusababisha ukame katika jiji hilo.
Katika hatua nyingine, Dk. Mpango alitembelea na kukagua bustani ya miche inayozalishwa na TFS eneo la Mailimbili Dodoma na kuuagiza wakala huo kuzalisha miche mingi zaidi na kuanzisha vitalu vipya vya miche kwa lengo la kuongeza kasi ya upandaji miti kwa wananchi wanaohitaji miche hiyo.
Alisema mpango wa serikali ni kuifanya Dodoma kuwa ya kijani na kuanzia mwakani kampeni hiyo inatarajia kubadili mwonekano wa mji huo.
NA MWANDISHI WETU, DODOMA



























