MRATIBU wa Chanjo kutoka Manispaa ya Ubungo, Hezron Msongole amewataka watanzania kupuuza upotoshaji unaofanywa na watu mbalimbali kuhusu chanjo ya Uviko 19 na badala yake wawe na imani na chanjo hiyo na wajitokeza kwa wingi kuchanjwa.
Msongole aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari ya jinsi ya kuripoti habari za afya ikiwemo za chanjo ya ziada za Uviko 19 yaliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa).
Alisema moja ya sababu ambayo inawafanya watanzania wengi kutopata chanjo ya Uviko 19 ni imani potofu iliyojengeka kichwani mwao kwamba chanjo hizo zina madhara jambo ambalo amesema kuwa si kweli.
“Hakuna ukweli kwamba chanjo hizi zina madhara, chanjo hizi ni muhimu kwa watu kuchanja ili kuweza kujikinga
Hata hivyo alisema kuwa wananchi 313,269 kutoa mkoa wa Dar es Salaam ambao walipata awali chanjo ya Uviko 19 hawakurudi tena kupata chanjo ya pili tangu chanjo hizo zilipoanza kutolewa mwaka 2021.
Aidha alisema jumla ya watu 2,271,698 walichomwa chanjo ya J&J ambayo uchomwa dozi moja huku waliochomwa chanjo ya Pfizer dozi ya kwanza wakiwa 822,090 lakini kati ya hao waliorudi kwa ajili ya chanjo ya pili ni 678,492.
“Chanjo ya Sinopharm waliochoma dozi ya kwanza ni 506,514 ila waliorudi kupata dozi ya pili ni 410,057 hivyo watu 96,457 hawakurudi kukamilisha dozi ya pili,” alisema na kuongeza
“Kwa upande wa chanjo ya Moderna waliochoma dozi ya kwanza ni 70,501 waliorudi kukamilisha dozi ya pili ni 50,156 hivyo watu 20,345 hawakukamilisha dozi, kwa chanjo ya Sinovac dozi ya kwanza walichoma watu 327,876 waliorudi kukamilisha dozi ni 275,007 hivyo watu 52,869 hawakurudi kukamilisha dozi ya pili,” alisema
Aidha alisema watu wanaweza kupatiwa dozi ya ziada ya chanjo dhidi ya Uviko 19 pale ambapo anakuwa amekamilisha ratiba yake ya awali na kwamba dozi hiyo ya ziada inatolewa baada ya miezi sita tangu pale mtu anakuwa amekamilisha ratiba ya chanjo za awali.
“Kwa chanjo ya Janssen dozi ya ziada itatolewa baada ya miezi sita toka mtu apate dozi ya kwanza, kwa chanjo za Sinopharm, Sinovac, Moderna na Pfizer mteja apatiwe dozi ya ziada baada ya miezi sita toka apate au Kukamilisha dozi ya pili”.alisema.