MIAKA 10 tangu kifo cha baba yake, mtoto wa kiume wa kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi, Seif al- Islam, ametangaza rasmi nia yake ya kugombea kiti cha Urais wa Libya katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Desemba, mwaka huu.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 49, amejitokeza na kuonekana katika mkanda wa video uliotolewa na ofisi inayosimamia uchaguzi, akitia saini nyaraka katika kituo cha uchaguzi kusini mwa mji wa Sebha.
Vyombo vya habari vya nchini Libya, vimeripoti kuwa katika video hiyo, Seif anayetajwa kuwa mmoja wa watu mashuhuri na mwanasiasa mtata, alisema Mungu pekee ndiye ataamua juu ya mustakabali wa taifa hilo na si mtu mwingine yeyote.
Baadhi ya wagombea wengine ni pamoja na kamanda wa kijeshi upande wa mashariki Khalifa Haftar, Waziri Mkuu Abdulhamid al-Dbeibah na Spika wa bunge Aguila Saleh.
Hata hivyo, wakati jina lake ni miongoni mwa majina yanayojulikana sana Libya na miongoni mwa watu waliokuwa na jukumu kubwa katika sera za nchi hiyo kabla ya vuguvugu la mwaka 2011, lililoungwa mkono na Jumuiya ya kujihami NATO na kuharibu utawala wa familia yake, Seif amekuwa nje ya macho ya umma kwa karibu muongo mmoja.
Kujitosa kwake rasmi katika kinyang’anyiro cha uchaguzi, ambao sheria zake bado zinapingwa na makundi tofauti ya Libya, kunaibua hoja mpya ya uchaguzi utakaomshirikisha mgombea anayeangaliwa katika baadhi ya mikoa kuwa asiyekubalika.
Licha ya umma wa Libya na mataifa ya kigeni kuunga mkono uchaguzi wa Desemba 24, mustakabali wa uchaguzi huo umesalia mashakani kwasababu ya kutokubaliana juu ya kanuni na ratiba ya uchaguzi.
Mkutano mkubwa juu ya Libya uliofanyika Paris wiki iliyopita, ulikubaliana juu ya kuweka vikwazo kwa yeyote atakayeingilia kura hiyo, lakini ikiwa zimebaki wiki sita kabla ufanyike, hakuna makubaliano yaliyofikiwa juu ya sheria za uchaguzi.
Changamoto nyingine inatajwa kuwa ni mpasuko mkubwa uliopo baina ya eneo la mashariki na magharibi, mgawanyiko uliotokana na vita ya muda mrefu na uwepo wa maelfu ya wapiganaji na mamluki wa kigeni.
Seif al-Islam alikamatwa na wapiganaji mwishoni mwa mwaka 2011, mwaka ambao baba yake aliondolewa madarakani kabla ya kuuwawa. Aliachiwa Juni mwaka 2017, baada ya kuwekwa kizuizini kwa zaidi ya miaka mitano.
TRIPOLI, Libya