POLISI imemtia mbaroni mtuhumiwa aliyefanya mauaji ya Katibu wa Halmashauri ya Walei ya Parokia ya Kanisa Katoliki Makambako, mkoani Njombe, Nickson Myamba Februari 7, mwaka huu.
Mtuhumiwa huyo, Daniel Mwilango, alikamatwa katika eneo la Doma, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.
Akitoa taarifa kuhusu kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issah, amesema mtuhumiwa alikamatwa akiwa safarini akielekea njia ya Njombe kwenye barabara ya Morogoro Mikumi.
Amesema kuwa baada ya kukamatwa mtuhumiwa huyo Februari 10, mwaka huu, alikutwa na vitu mbalimbali ikiwemo simu ya marehemu Nickson Myamba, funguo mbalimbali ikiwa ni pamoja na za chumba ambacho tukio hilo la mauaji lilitekelezwa.
Kamanda Issah amesema kuwa baada ya polisi kuendelea na upelelezi wao mjini Makambako, walikuta kufuli ambayo ufunguo wake alikuwa nao mtuhumiwa.
“Ni dhahiri bila chenga huyu mtuhumiwa anahusika na hili tukio na vitu vyote anavyo na katika mahojiano kabla ya hapo, mtuhumiwa alipofikishwa hapa kituo cha polisi Makambako aliweza kueleza yeye mwenyewe panga lilikuwa wapi na limepatikana katika shimo la choo Shule ya Msingi Makambako, kingine alichoweza kukionyesha mtuhumiwa ni chuma ambacho alimpiga nacho marehemu,” amesema.
Aidha, Kamanda Issah, akielezea tukio hilo lilivyotekelezwa alidai mtuhumiwa alimpiga Myamba na chuma kizito kichwani, kisha alitenganisha kiwiliwili vipande viwili na kuviweka ndani ya mifuko ya nailoni na kusafisha kwa maji damu iliyokuwa imetapakaa ndani ya chumba cha duka kwenye eneo la kanisa hilo.
“Baada ya kumpiga Myamba, Daniel alichokifanya aliamua kutumia panga katika kuutenganisha kiwiliwili, alitenganisha kichwa na kifua kilikuwa sehemu yake na kiuno na miguu ilikuwa sehemu yake, aliendelea na kuchukua kipande cha kichwa cha marehemu na kifua na kukiweka kwenye salfeti na mwili uliweza kuhifadhiwa ili damu isiweze kutiririka,” alisema.
Alidai kisha mtuhumiwa huyo alichukua boksi na kulitumia katika kuweka kiwiliwili cha kiuno na miguu, alifunga mlango wa chumba cha duka na kutafuta mbinu za kuutoa huo mwili uliokuwa ndani ya boksi.
Hata hivyo, kamanda huyo alidai mtuhumiwa hakufanikiwa kuutoa mwili huo badala yake alielekea nyumbani kwake ambapo aliaga na kuondoka.
Kamanda Issah alisema jeshi lake pia linamshikilia mlinzi wa Kanisa Katoliki Makambako, Nickson Valentine kwa kumshuku kushiriki katika tukio hilo.
“Bado upelelezi unaendelea, lakini kwa hali ya sasa hivi mtuhumiwa aliyefanya tukio hilo ametiwa mbaroni, tunapenda kuwapongeza baba paroko na viongozi wake wa kanisa na wananchi wa Makambako na askari wa jeshi la polisi kwa kushirikiana vizuri katika kuhakikisha hili jambo tunalipatia ufumbuzi,” alisema.
Kutokana na mauaji hayo kuhusisha viongozi wa kanisa hilo, Paroko wa kanisa hilo Padri Pascal Makoha alilipongeza jeshi la polisi kwa kufanikisha kumkamatwa kwa mtuhumiwa huyo, huku akiwasihi waumini wa kanisa hilo waendelee kuwa na subira wakati vyombo vya dola vikiendelea na upelelezi.
“Hali katika kanisa letu ipo shwari, tunashukuru jeshi la polisi, hapa kanisani tunaendelea na Novena ya siku tisa, tunawaomba waumini waendelee kuja bila hofu yoyote, tendo hili limetendwa na watu wachache au mtu mmoja ambaye alikuwa na nia mbaya, lakini kanisa kama kawaida linatetea uhai wa binadamu,” alisema.
Na MICHAEL KATONA, Njombe



























