Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akishuka ndani ya Basi aina ya Tata linalofanya kazi ya kubeba wanafunzi Mjini Shinyanga.
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa hatua mbalimbali inazofanya katika kutekeleza usimamizi wa kuzuia na kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kwa kununua magari mawili yanayobeba wanafunzi kuwapeleka shuleni na kuwarudisha karibu na makazi yao.
Waziri Dkt. Gwajima ametoa pongezi hizo leo Jumatatu Desemba 5,2022 wakati akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Town baada ya kupanda gari moja na wanafunzi hao kutoka majumbani mwao kuelekea katika shule hiyo iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga ikiwa ni ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia
“Nawapongeza sana Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa ubunifu huu wa usafiri kwa gharama nafuu shilingi 200 kutoka nyumbani hadi shuleni, nina imani wanafunzi sasa watatumia muda mfupi kwenda shuleni na kuwaepusha na vishawishi mbalimbali wawapo njiani, lakini nimeshuhudia gari hili likiwa na Msimamizi wa wanafunzi ambaye ni Afisa Maendeleo ya jamii, hii ni hatua nzuri sana, ni vyema Halmashauri zingine zikaiga mfano wa Manispaa ya Shinyanga namna ya kusaidia wanafunzi, zisisubiri matamko”,amesema Dkt. Gwajima.
Katika hatua nyingine Dkt Gwajima amezitaka halmashauri na Mikoa yote nchini kuandaa mifumo ya upatikanaji wa haraka wa taarifa za kulinda watoto utaosaidia kufahamu taarifa za watoto.
“Mtengeneze na mifumo itakayogundua iwapo mtoto hayupo shuleni, iunganishwe kuanzia wazazi, walimu, polisi na jamii nzima. Endapo tutakuwa na mfumo wa kulinda watoto itatusaidia pia kudhibiti utoro shuleni, tutaweza kutambua kama mtoto yupo shule au la! Wazazi pia watasaidia kujua mtoto yuko wapi. Mfumo wa pamoja wa taarifa utasaidia kupata sulushisho la matukio ya ukatili katika jamii”, amesema.
Katika hatua nyingine amewataka wadau kuendelea kupaza sauti juu ya vitendo vya jinsia moja huku akibainisha kuwa hatakubali kuona vitendo vya ushoga na vitendo vingine vya ukatili wa kijinsia kwenye vyombo vya usafiri vinavyobeba wanafunzi lakini pia shuleni.
“Suala la mapenzi ya jinsia moja halitafumbiwa macho kwa namna yoyote ile, watoto watalindwa kwa hali zote. Nawatangazia waovu wote wanaofundisha madarasa ya ushoga waache mara moja, hata huyo mwanaume aliyekamatwa huko Geita akifundisha watoto ushoga akiwa amevaa nguo za kike ‘sidiria’ na vitu vya kike kike ni lazima achunguzwe, tutalifuatilia hili jambo haiwezekani watoto wetu waharibiwe kwa kufundishwa mambo yasiyofaa, Hili la ushoga nitalifia. Tutawalinda watoto, na hayo madarasa ya ushoga yafe huko huko”,amesema Dkt. Gwajima.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Prof. Siza Tumbo amesema ameahidi mkoa huo kuendelea kupambana na vitendo vya ukatili na kufuata maelekezo yote yaliyotolewa na kwamba wamejipanga kukutana na wadau mbalimbali ili kutengeneza mfumo wa kutoa taarifa kwa ajili ya kuwalinda watoto.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manipaa ya Shinyanga, John Tesha ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga, amesema halmashauri hiyo inaendelea kutoa elimu ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto mara kwa mara katika ngazi ya jamii, kwenye nyumba za ibada na Shule za msingi , Sekondari na vyuo.
“Pia halmashauri imetumia nafasi ya utoaji mikopo kwa asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kama njia nyingine za kuzuia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto”,amesema Tesha.
“Mfano mwingine wa namna mikopo ya asilimia 10 ilivyosaidia kwenye kuzuia na kutokomeza ukatili kwa watoto ni ule ambao mwezi Aprili 2022, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi Milioni 120 kwa vikundi viwili vya vijana. Vikundi hivyo tulivisimamia na kununua magari mawili (Moja ni Basi aina ya Tata na lingine ni Basi dogo aina ya Nissan – Civilian) yanayofanya kazi ya kubeba wanafunzi”,ameongeza Tesha.
Ameeleza kuwa Vikundi hivyo vya vijana vilipewa maelekezo na kusainiana mkataba na Halmashauri kuhakikisha nyakati za asubuhi kuanzia saa 12 hadi saa 2 asubuhi magari hayo yanabeba wanafunzi kuwapeleka shuleni na nyakati za jioni kuanzia saa 10 na nusu hadi saa 12 jioni magari hayo yanabeba wanafunzi kuwarudisha karibu na makazi yao kwa bei elekezi ya shilingi 200/= / 300/=.
“Lengo la kufanya hivi ni kuwahakikishia wanafunzi usalama wao wanapoenda shuleni na wakati wa kurudi nyumbani na kuhakikisha wanafunzi wanafika shuleni kwa wakati na siku zote za masomo hivyo kuwahakikishia ufaulu mzuri katika mitihani yao”,amesema Tesha.
Amesema upatikanaji na utumiaji wa magari hayo ya mkopo kwa vijana yamewapunguzia wazazi gharama za kuwasafirisha watoto kwenda na kurudi shuleni ambapo gharama za kumsafirisha mtoto kwenda na kurudi shuleni kwa siku ni kati ya shilingi 500/= – 600/= na kwa mwezi ni kati ya shilingi 10,000/= – 12,000/=
“Hii ni gharama nafuu ukilinganisha na gharama walizokuwa wanatumia wengi wao za kutumia baiskeli ambapo huwa ni shilingi 500/= hadi 1000/= kwa safari moja ambapo kwa siku ni shilingi 1000/= -hadi 2000/= na kwa mwezi ni shilingi 20,000/= hadi 40,000/=”,ameeleza.
“Kwa kutumia mikopo ya asilimia 10 pia Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imetoa Bajaji kwa watu wenye ulemavu kwa ajili ya biashara ya usafirishaji wa abiria ambapo pia waliokopa tumewaelekeza kubeba wanafunzi popote wanapowakuta kwa bei elekezi. Pia katika mwaka huu wa fedha 2022-2023 unaoendelea tumejipanga kutoa mikopo ambayo itawezesha kununua magari/ Hiace Sita ambazo zitawajibika kufanya biashara ya abiria ndani ya Manispaa na kuhakikisha zibabeba wanafunzi kwa bei elekezi”,amefafanua Tesha.
Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Taifa Nancy Kasembo ameshukuru uongozi wa mkoa na Manispaa ya Shinyanga kwa ubunifu huo ambao utasaidia kupunguza utoro na mimba za utotoni kutokana na ukatili.
Akiwa mkoani Shinyanga Waziri Gwajima amezungumza pia na wananchi kupitia kituo cha Redio Faraja Fm, kufanya mazungumzo na Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu pamoja na kutembelea Kamati ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto kata ya Ibinzamata sambamba na kutoa vyeti vya pongezi kutambua mchango wa baadhi ya taasisi na watu binafsi katika kushiriki mapambano dhidi ya ukatili kwa wanawake na watoto.
Baadhi ya waliokabidhiwa vyeti hivyo ni Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga Tedson Ngwale, Mwandishi wa Habari wa Azam Tv Kasisi Kosta , Chama cha waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club -SPC), ICS, kituo cha Redio Faraja Fm ,Doctors with Africa (CUAMM) ICS-Creating change na Shinyanga EVAWC Working group
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akisalimiana na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Town Manispaa ya Shinyanga kabla ya kupanda kujionea namna Basi la Wanafunzi linavyosafirisha wanafunzi Mjini Shinyanga leo Jumatatu Desemba 5,2022.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akisalimiana na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Town Manispaa ya Shinyanga kabla ya kupanda kujionea namna Basi la Wanafunzi linavyosafirisha wanafunzi Mjini Shinyanga. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manipaa ya Shinyanga, John Tesha ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga.