KIUNGO wa timu ya Yanga, Mukoko Tonombe, ameahidi kufanya mazoezi ya nguvu ili kuhakikisha anapambana katika vita ya namba kucheza katika kikosi cha kwanza na mpinzani wake Khalid Aucho.
Mukoko ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Aucho raia wa Uganda wamekuwa katika upinzani mkali wa kuwania namba kikosi cha kwanza katika msimu huu.
Hata hivyo, Mukoko amekuwa akiwekwa benchi mara nyingi kutokana na Kocha wa Yanga Nasreddine Nabi kumtumia zaidi Aucho.
Katika michezo mitano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Mukoko amecheza mchezo mmoja dhidi ya Ruvu Shooting huku Aucho akicheza michezo minne nne.
Kocha Nabi, katika eneo la kiungo amekuwa akiwatumia zaidi Yanick Bangala, Feisal Salum na Aucho, huku Zawadi Mauya na Mukoko wakisubiri katika benchi.
Akizungumza na UhuruOnline, Mukoko alisema amejipanga kujituma zaidi katika mazoezi na kumvutia kocha kumpa namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Alisema licha ya ushindani wa namba kuwa mkali kila kukicha, lakini ana imani mazoezi anayoyafanya kwa sasa yatamsaidia kufikia malengo aliyojiwekea ya kupata namba ya kudumu kikosini.
“Natamani ligi ianze kuanza hata kesho (leo) ili nipate nafasi ya kucheza na kuonyesha uwezo wangu kwani lengo langu kubwa msimu huu ni kuhakikisha ninabeba tuzo ya mchezaji bora wa msimu, ndio maana napambana kuhakikisha napata nafasi ndani ya kikosi cha kwanza.
“Upinzani wa namba kwa sasa ni mkali kila mchezaji anataka kuonyesha makali yake ili kupata nafasi kikosini, hivyo nitaendelea kujituma zaidi mazoezini na kumshawishi kocha kunipa nafasi,” alisema Mukoko.
Mukoko alisema kwa sasa amekuwa akifanya mazoezi makali na kujituma zaidi, ili kuhakikisha anaendelea kuimarika kabla ya Ligi Kuu Tanzania Bara haijarejea.
Yanga ilianza Ligi kwa kupata ushindi wabao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, ikashinda 1-0 dhidi ya Geita Gold, wakaichabanga mabao 2-0 KMC, wakashinda mabao 2-0 mbele ya Azam FC kabla ya kuitandika Ruvu Shooting mabao 3-1.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ipo kileleni ikiwa na pointi 15 na kushuka dimbani mara tano ambapo imefunga mabao tisa huku ikiruhusu kufungwa bao moja pekee.
Na NASRA KITANA