SERIKALI imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2022, lengo likiwa kuweka mfumo tulivu wa kodi wenye kutabirika, kuboresha taratibu za ulipaji, ukusanyaji kodi, kuimarisha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini.
Muswada huo umelenga kufanya marekebisho ya sheria 35 zinazohusu fedha, kodi, ushuru na tozo kwa lengo la kuweka, kurekebisha, kupunguza au kufuta viwango vya kodi, ushuru, ada na tozo.
Akiwasilisha muswada huo bungeni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema umezingatia maoni ya wabunge na wataalamu.
“Kufuatia majadiliano na wadau mbalimbali hususan michango ya wabunge wakati wakijadili bajeti ya serikali kwa mwaka 2022/23 na maoni ya Kamati ya Bunge ya Bajeti, serikali imefanya marekebisho mbalimbali ya hatua za mapato zilizowasilishwa kupitia hotuba ya bajeti,” alisisitiza.
KODI MBALIMBALI
Dk. Mwigulu alisema hatua ya kwanza iliyochukuliwa ni kupunguza kiwango cha kodi katika zawadi ya ushindi kutoka asilimia 15 hadi asilimia 10 katika michezo ya kubahatisha ya ubashiri wa matokeo ya michezo.
Alisema lengo la hatua hiyo ni kuongeza mapato ya serikali kutokana na watu wengi zaidi kuhamasika kushiriki michezo ya kubahatisha ya kubashiri matokeo.
“Uchambuzi uliofanyika umebainisha endapo serikali itaendelea kupunguza kiwango husika hadi kufikia asilimia 10, mapato ya serikali yataongezeka kutoka sh. bilioni 4.2 hadi sh. bilioni 5.2, kutokana na watu wengi kuhamasika kushiriki katika michezo hiyo,” alibainisha.
Pia, Dk. Mwigulu alisema serikali imeamua kutofanya marekebisho ya kubadili mgawanyo wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ili kuhudumia miundombinu ya masoko ya machinga.
Alisema serikali itatumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali katika bajeti ya mwaka 2022/23 ambazo ni sh. bilioni moja kwa kila mkoa kwa halmashauri za majiji na manispaa zitumike kujenga miundombinu na masoko ya machinga.
Katika muswada huo, serikali imeondoa pendekezo la kutoza kodi ya zuio kwa kiwango cha asilimia mbili katika malipo ya wachimbaji wadogo wa madini.
Alisema utozaji wa kodi husika ungesababisha utoroshaji madini na kupunguza kasi ya wachimbaji kuuza madini katika masoko rasmi au vituo vya uchenjuaji.
Mbali na hizo, nyingine alisema serikali imeondoa hatua ya kutoza kodi ya awali ya mapato ya sh. 20 kwa lita kwa wafanyabiashara wa rejareja wa mafuta ya petroli nchini ambayo ingekusanywa na waingizaji wa mafuta kwa jumla kisha kulipwa serikalini.
Aidha, Dk. Mwigulu alisema serikali imefanya maboresho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kusamehe kodi hiyo katika mafuta ya kula yanayozalishwa nchini kwa kutumia mbegu zinazozalishwa ndani.
Alisema hatua hiyo itahusisha kusamehe kodi katika malighafi na vifungashio vinavyotumika katika uzalishaji mafuta hayo.
MABADILIKO TASAC
Waziri huyo alisema serikali imefanya uamuzi wa kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ili taasisi hiyo isijihusishe na jukumu la uwakala wa forodha, badala yake ibaki na jukumu la kusimamia na kudhibiti watoa huduma za usafiri majini.
Hata hivyo, alisema taasisi hiyo itaendeleza shughuli za uwakala wa forodha katika bidhaa za makinikia, silaha, vilipuzi, nyara za serikali na wanyama hai wanaotambulika kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori.
Alifafanua hatua hiyo itaondoa mgongano wa maslahi unaotokana na TASAC kuwa mtoa huduma za uwakala wa forodha na mdhibiti wa watoa huduma za usafiri majini kwa wakati mmoja.
Dk. Mwigulu alisema serikali inapendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Ardhi, Sura 113 ili kuweka utaratibu kwa waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha baada ya kufanya mashauriano na waziri mwenye dhamana ya masuala ya ardhi, mamlaka ya kusamehe riba ya malimbikizo ya pango la ardhi.
Alieleza lengo la hatua hiyo ni kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari na kuongeza mapato ya serikali kwa kukusanya malimbikizo ya kodi husika.
NEEMA ELIMU YA JUU
Katika marekebisho hayo, alisema serikali inakusudia kuongeza wigo wa kusamehe tozo ya mafunzo ya ufundi stadi kwa wahitimu wa elimu ya juu na vyuo vya kati, badala ya vyuo vikuu pekee kama ilivyopendekeza awali katika hotuba ya bajeti.
Waziri Mwigulu alisema lengo la hatua hiyo ni kuongeza idadi ya wanufaika wa mafunzo ya vitendo ya kuwapatia ujuzi na uzoefu wa kazi kabla ya ajira kupitia Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA).
Pia, alisema serikali itasogeza muda wa kufutwa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani katika huduma za kukodi ndege kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai mosi, mwaka huu, kutoa fursa ya utekelezaji wa miadi iliyowekwa kwa kuzingatia uwepo wa msamaha huo.
SHERIA ZILIZOPENDEKEZWA
Awali, Dk. Mwigulu alizitaja sheria zilizopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni Sheria ya Magonjwa ya Wanyama, Sura ya 156, Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sura ya 197, Sheria ya Usajili wa Majina ya Biashara, Sura ya 213 na Sheria ya Korosho, Sura ya 203. Alizitaja zingine ni Sheria ya Usajili wa Kampuni, Sura ya 212, Sheria ya Hakimiliki, Sura ya 218, Sheria ya Tasnia ya Maziwa, Sura ya 262, Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura ya 147, Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura ya 306 na Sheria ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, Sura ya 414.
Zingine ni Sheria ya Usafirishaji Bidhaa Nje ya Nchi, Sura ya 196, Sheria ya Mbolea, Sura ya 378, Sheria ya Magari ya Kigeni, Sura ya 84, Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura ya 41, Sheria ya Mikopo ya Serikali, Dhamana na Misaada, Sura ya 134, Sheria ya Ngozi na Bidhaa za Ngozi, Sura ya 120 na Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332.
Waziri huyo alizitaja sheria nyingine zinazopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni Sheria ya Bima, Sura ya 394, Sheria ya Ardhi, Sura ya 113, Sheria ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Nchi Kavu, Sura ya 413, Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287.
Zingine ni Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288, Sheria ya Madini, Sura ya 123, Sheria ya Mifumo ya Malipo, Sura ya 437, Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Sura ya 297, Sheria ya Bandari, Sura ya 166, Sheria ya Uwekezaji, Sura ya 38, Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Sura ya 399 na Sheria ya Wakala wa Meli, Sura ya 415.
Kwa mujibu wa Dk. Mwigulu, zingine ni Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura 438, Sheria ya Rufani za Kodi, Sura ya 408, Sheria ya Usajili wa Wadhamini, Sura ya 318, Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148 na Sheria ya Mafunzo na Ufundi Stadi, Sura ya 82.
Na MUSSA YUSUPH, Dodoma