Na HAWA NGADALA
MWALIMU Zakia Khatibu wa Shule ya Msingi Jangwani, Dar es Salaam, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni, kujibu shitaka la kumsababishia majeraha mabaya mwanafunzi kwa kumpiga kofi jichoni.
Zakia (34), alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Shindai Michael, mbele ya Hakimu Mkazi, Aaron Lyamuya.
Wakili Shindai alidai Novemba 21, mwaka 2019, eneo la Shule ya Msingi ya Jangwani, iliyoko Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, mshitakiwa huyo alimpiga kofi mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa) kwenye jicho la kushoto na kumsababishia majeraha.
Mshitakiwa alikana shitaka hilo, ambapo upande wa jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kumsomea maelezo ya awali.
Akimsomea maelezo hayo, Shindai aliieleza mahakama kuwa mshitakiwa Zakia ni mwalimu wa Shule ya Msingi Jangwani.
Alidai Novemba 21, mwaka 2019, mshitakiwa akiwa darasani alimpiga kofi mwanafunzi huyo katika jicho lake la kushoto na kumsababishia jeraha la kudumu na hatimaye alifikishwa mahakamani hapo Machi 16, mwaka huu na kusomewa shitaka.
Baada ya kusomewa maelezo hayo, mshitakiwa huyo alikubali maelezo hayo isipokuwa kumpiga kofi na kumsababishia jeraha la kudumu.
Hakimu Lyamuya alimtaka mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, ambao watatia saini dhamana ya sh. milioni tano.
Upande wa jamhuri ulidai kwamba unategemea kuwa na mashahidi 12 ambapo April 12, mwaka huu, shahidi namba moja ataanza kutoa ushahidi na mshitakiwa yupo nje baada ya kufanikiwa kutimiza masharti ya dhamana.