Na NASRA KITANA
KOCHA wa Yanga, Juma Mwambusi amesema ataiongoza timu kwa kutekeleza mambo makuu matatu ili kufanikisha malengo ambayo yaliwekwa na uongozi mwanzoni mwa msimu.
Mwambusi ametoa kauli hiyo saa chache baada ya uongozi wa Yanga kumkabidhi timu timu hadi mwisho wa msimu huu.
Kocha huyo alipewa timu Machi 9, mwaka huu, kama kocha wa muda baada ya Mrundi, Cedric Kaze na wasaidizi wake wa benchi la ufundi kufutwa kazi.
Kaze aliondolewa pamoja na Kocha Msaidizi, Nizar Khalfan, Vladimir Niyonkuru, Edem Mortoisi na Ofisa Usalama wa timu, Mussa Mahundi.
Benchi hilo lilifumuliwa saa chache baada ya Yanga kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Polisi Tanzania huku mwenendo mbaya wa timu ukiwa sababu kuu ya viongozi wa benchi hilo kutimuliwa.
Akizungumza jana, Mwambusi alisema baada ya kupewa timu jambo la kwanza aliloanza kulifanya ni kuhakikisha timu inakuwa na muunganiko mzuri ambao haukuwepo kutokana na mifumo ya makocha waliopita.
Mwambusi alisema timu ina wachezaji wengi wa kigeni ambao hadi sasa hawajazoea mfumo wa uchezaji na ndio maana timu haifanyi vizuri kama inavyotakiwa hivyo hana budi kuwasimamia kuhakikisha wanazoea mfumo na kutimiza wajibu wao kikamilifu.
Alisema kuwa kipaumbele cha pili ni kuhakikisha timu inaendelea na moto wa kusaka ubingwa licha ya kuwa ushindani unaongeza kila uchao.
“Nimepewa timu wiki iliyopita lakini siwezi kusema Yanga haitatwaa ubingwa, nafasi bado ipo na nitahakikisha naiongoza ili kufanikisha malengo ambayo yaliwekwa tangu kuanza kwa msimu,” alisema Mwambusi.
Pia, kocha huyo alisema hatakubali kupoteza mechi zilizobaki ikiwemo ya watani wa jadi itakaofanyika Mei 8, mwaka huu.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema kuwa licha ya Mwambusi kukabidhiwa timu hadi mwisho wa msimu huu huku mchakato wa kupata kocha mpya unaendelea.
“Mwambusi ataendelea kukinoa kikosi chetu hadi msimu utakapoisha huku tukiendelea kusaka kocha mpya kwa utulivu na hata akipatikana basi atajiunga na timu msimu ujao,” alisema Bumbuli.
WACHAMBUZI WATOA NENO
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wachambuzi wa soka wameupongeza uongozi wa Yanga kwa kumpa kocha mazawa timu.
Nyota wa zamani Ali Mayai alisema Yanga imefanya uamuzi mzuri na kurudisha imani ya makocha wazawa.
Mayay alisema makocha wazawa wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi iwapo watazidi kuaminiwa.
“Mwambusi anaijua vyema Yanga, naamini kuwa ataipa matokeo mazuri timu ambayo ina nafasi nzuri ya kutwaa taji,” alisema.
Kocha anatakiwa kuwa mzoefu na awe ameizoea timu ila akiingia tu na kukabidhiwa timu ikiwa kwenye mashindano ni jambo la muda kupata matokeo mazuri,” alisema Mayai.
Alex Kashasha alisema Yanga inaweza kuwa bora zaidi katika mechi zitakazofuata kutokana na uwezo wa Mwambusi.
Kashasha alisema kuwa kama kocha huyo atayatekeleza kikamilifu maazimio aliyojiwekea timu hiyo itwaa ubingwa.
Kocha huyo amewahi kufundisha timu za Mbeya City kama kocha mkuu, Singida United, Yanga na Azam akiwa kocha msaidizi.