“NILISHANGAA nilivyomuona binti wa kimasai akipata tabu sana na kujigagalaza katika ardhi kutokana na matatizo ya tumbo la hedhi, kukosa kwenda shule kutokana na kukosa taulo za kike nilihuzunika na nikaamua kutengeneza taulo za kike za kufua ili binti aende shule na kupata masomo yake,” anasema Mwanaidi.
Mwanaidi ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Jolloe ambayo inajishughulisha na utengenezaji taulo za kike za kufua.
Mjasiriamali huyo anasema alianza kazi hiyo mwaka 2019 baada ya kushuhudia binti akipata tabu na kukosa masomo kutokana na kukosa taulo za kike.
Anasema baada ya kupata ushuhuda huyo ndiyo sababu ya kuanzisha kampuni hiyo ya Jollie yenye lengo la kusaidia wanawake na binti kuepukana na tatizo la hedhi.
“Baada ya kuona hivyo nikaamua kufuatilia taratibu za vitambaa ambavyo nitatengeneza kwa ajili ya taulo za kufua, nilienda nchini Kenya kwa lengo la kupata bidhaa ambazo nitatengeneza.
“Nilipata chache ila nashukuru nilipata watu ambao walielekeza kuwa zinapatika China, ndiyo nikafunga safari ya kwenda huko kwa ajili ya kupata bidhaa hizo kwas sababu hapa nchini kupatikana ni tabu sana,” anasema Mwanaidi.
Mjasiriamali huyo anaelezea baada ya kufanikisha taulo za kike za kufua za kwanza alimpelekea yule binti ya kimasai kwa ajili ya kufanya majaribio.
Mwanaidi anafafanua kuwa majaribio yalikuwa mazuri, kutokana na yule binti kufurahia zile taulo za kike za kufua. kufanikiwa kwenda shule hata akiwa yupo katika hedhi.
“Nashukuru Mungu jaribio lilienda vizuri, baada ya kumpelekea yule binti wa kimasai niliwapelekea wanafunzi wa shule za mikoani Kigoma, Pwani na Tanga,” anasema Mwanaidi.
Mjasiriamali huyo anasema licha ya kutengeneza taulo za kike za kufua kupitia kampuni yake ya Jollie hata hivyo inajihusisha na kutoa elimu ya hedhi kwa wasichana na kufahamu umuhimu wao katika jamii.
Anasema wasichana wengi wanapata tabu na kunyanyasika kipindi cha hedhi, wameanzisha kundi liitwalo Udada Club ambao unasaidia kutoa elimu ya hedhi na umuhimu wa msichana katika jamii.
FAIDA ZA TAULO ZA KIKE ZAKUFUA
“Taulo za kike zinazofuliwa sifa faida nyingi ukitumia unaepukana na maradhi nyemelezi ya bacteria, pia rahisi kutumia mahali popote ile,” anasema.

Mwanaidi anasema taulo ya kufua ukinunua mara ya moja unatumia miaka miwili kutokana na staili yake ya kuvaa na kufua.
“Ukinunua taulo hizi za kike unahifadhi ela kwa sababu ni bidhaa ambalo unanunua mara moja na kutumia kwa miaka miwili bila kununua nyingine, toafuti na taulo za kutupa,” anasema.
MAFANIKO
Mwanaidi anasema kazi hiyo imefungulia milango mingi ya kujulikana na sekta mbalimbali za kutangaza biashara hiyo ndani na nje ya nchi.
Anasema kazi hiyo sasa inatambulika na serikali na sekta tofauti ambazo zinatarajia kufanya naye biashara na kutoa elimu juu ya umuhimu wa taulo za kufua.
“Nashukuru Mungu faida zimeanza kuonekana japokuwa bado kifedha sijaanza kuona matunda yake, ila kwa hapa nilipofikia nashukuru.
“ Kujulikana na serikali ni jambo kubwa na kuunga mkono juhudi zako kwangu ni faida kubwa,” anasema.
TOFAUTI YA TAULO ZA KIKE ZIZOFULIWA NA TAULO ZA KIKE ZINAZOTUPWA
Mjasiriamali huyo anaeleza kuwa kuna tofauti kubwa kati ya taulo za kike zinazofuliwa na taulo za kike zakutupa ”Taulo za kike zakufuliwa hazina kemikali, zaidi ya ukimaliza kutumia unafua, tofauti na taulo za kike zakutupa zile zinatengenezwa na plastini na kuwekwa kemikali,” anasema.
Pia, Taulo za kike zakufuliwa unatumia kwa muda mrefu bila kupata gharama tofauti na taulo za kike zakutupa unatumia gharama nyingi kila mwezi.
USHAURI TAULO ZA KIKE ZAKUFULIWA
Mwanaidi alitoa ushauri kwa wanawake kutumia taulo za kike zakufuliwa ili kuepukana na maradhi mbalimbali yanayotokana na bakteria.
“Ukitumia taulo za kike zinazofuliwa unakuwa na hedhi salama, pia upo sahihi kiafya wala haupati maradhi yanayotokana na bakteria za hedhi, pia watu ambao wana imani potofu kuwa mtu ukiwa katika hali ya hedhi apaswi kufanya kazi wala kupika hiyo sio kweli,” anasema.
Mjasiriamali huyo ameeleza ukitumia taulo za zakufuliwa unakuwa uhuru na salama kufanya kazi.
Na AMINA KASHEBA