MWILI wa mwanaharakati wa muda mrefu dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, Askofu Desmond Tutu, utaagwa kitaifa kwa siku mbili kabla ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika Januari mosi 2022, Jijini Cape Town.
Taarifa hiyo imetolewa na wakfu wa mwanaharakati huyo aliyekuwa pia kiongozi wa kidini na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel aliyefariki dunia Jumapili iliyopita akiwa na umri wa miaka 90.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ilieleza kuwa kabla ya kufikia uamuzi huo, awali mwili wa Tutu ungeagwa kitaifa kwa siku moja lakini mabadiliko yamefanyika na kuongeza siku ya pili kuanzia keshokutwa ili kutoa nafasi kwa watu wengi zaidi kutoa heshima za mwisho.
Leo, kulikuwa na ibada ya taifa mjini Pretoria ya kukumbuka mchango wa mwanaharakati huyo aliyeshirikiana na wengine akiwemo hayati Nelson Mandela, kupinga ubaguzi wa rangi ulioshamiri enzi ya utawala wa wazungu wachache nchini Afrika Kusini.
Desmond Mpilo Tutu alizaliwa mwaka 1931 katika mji mdogo wenye migodi ya dhahabu wa Transvaal.
Alifuata nyayo za baba yake kwa kuwa mwalimu kabla ya kuwacha kazi hiyo baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Elimu ya Bantu mwaka 1953 ambayo ilipalilia ubaguzi wa rangi shuleni.
Baada ya hapo alijiunga na kanisa kutokana na ushawishi mkubwa kutoka kwa viongozi weupe wa dini nchini humo hususan Askofu Trevor Huddleston aliyepinga ubaguzi wa rangi.
Alihudumu kama askofu wa Lesotho kuanzia 1976-78, askofu msaidizi wa Johannesburg na mkuu wa parokia ya Soweto, kabla ya kuteuliwa kuwa askofu wa Johannesburg.
Tutu alianza kupaza sauti yake dhidi ya ukosefu wa haki nchini Afrika Kusini kuanzia mwaka 1977 alipokuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa la Afrika Kusini.
Akiwa mtu mashuhuri kabla ya uasi wa 1976 katika vitongoji vya watu weusi, ilikuwa miezi kadhaa kabla ya matukio ya ghasia za Soweto ambapo alijulikana kwa mara ya kwanza na Wazungu wa Afrika Kusini kama mwanaharakati wa mageuzi.
Juhudi zake zilimfanya kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 1984 katika kile kilichoelezwa kuwa pingamizi kuu dhidi ya jumuiya ya kimataifa kwa watawala weupe wa Afrika Kusini.
Akiwa mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini Afrika Kusini, aliendelea kufanya kampeni kikamilifu dhidi ya ubaguzi wa rangi mwaka 1988 alinusurika kifungo gerezani baada ya kutoa wito wa kususia uchaguzi wa manispaa.
PETROLIA, Afrika Kusini