Na NASRA KITANA
LICHA ya kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mwadui FC, Kocha wa Yanga Nasreddin Nabi, amesema hajafurahishwa na kiwango walichoonyesha wachezaji wake, katika mchezo huo uliopigwa wikiendi iliyopita dimba la Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza kuhusu mchezo huo, Nabi amesema wamepata ushindi lakini ameona ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha maeneo yenye mapungufu yanafanyiwa kazi haraka ili kuongeza ushindani wa timu yake dhidi ya wapinzani wao.
Nabi amesema, amekuwa akiwapa mbinu tofauti wachezaji hao, lakini hawajaweza kutekeleza kile ambacho anawaagiza kitendo ambacho hakimfurahisha.
“Tumepata ushindi lakini sijafurahishwa na kiwango ambacho wachezaji wangu wamekionyesha, hivyo nitahakikisha nawajenga upya wachezaji wangu ili waweze kucheza soka safi na lenye kuvutia,” amesema Nabi.
Kocha wa Mwadui FC ya Shinyanga, Salhina Mjengwa, amesema licha ya timu yao kushuka daraja, pia lengo lao kubwa lilikuwa ni kuonyesha uwezo wa kikosi chao kwa kuifunga Yanga, na hilo lilishindikana.
Amesema waliingia uwanjani kwa lengo moja la kupata ushindi, lakini umakini mdogo uliwafanya wachezaji wake kubweteka na kushindwa kuzua mashambulizi.
“Tumesikitishwa na matokeo tuliyoyapata kwani hatukutarajia kupata matokeo haya, licha ya timu yangu kushuka daraja ila ndio mpira imebidi tukubali matokeo,” amesema Mjengwa.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 67, baada ya kushuka dimbani mara 31 huku Mwadui FC ikiburuza mkia kwa pointi 19 ikishuka dimbani mara 32.