KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema atayatumia mashindano ya Kombe la Mapinduzi kuangalia viwango vya wachezaji wake wapya watakaosajiliwa katika dirisha dogo msimu huu.
Yanga ikimalizana na Dodoma Jiji Jumamosi hii katika Ligi Kuu Tanzania Bara itasafiri kwenda Zanzibar kucheza michuano ya Kombe la Mapinduzi itakayoanza Januari 2, mwakani.
Vinara hao wa Ligi Kuu Bara ni moja ya timu kumi zitakazocheza michuano hiyo yenye lengo la kuyaenzi Mapinduzi matukufu ya Zanzibar yanayoadhimishwa Januari 12, kila mwaka.
Katika kombe hilo, Yanga imepangwa kundi B na timu za KMKM na Taifa Jang’ombe za Zanzibar.
Akizungumza jijini Dar es salaam, kocha Nabi, alisema anatamani kuona timu yake ikifanya vizuri katika michuano hiyo.
Alisema anatafuta njia bora ya kupumzisha wachezaji wa waliotumika sana msimu huu bila ya kuuathiri ubora wa kikosi chake katika michuano hiyo inayofanyika visiwani Zanzibar.
“Nina wachezaji ambao wamecheza sana katika mechi zetu za ligi kuu, nafikiria kuwapumzisha wachezaji hao katika mashindano ya mapinduzi, siyo kwamba nadharu mashindano hayo lakini nataka kuwapa nafasi wachezaji wengine ambao hawapati nafasi lakini pia niangalia viwango vya wachezaji wetu wapya watakaosajiliwa ndani ya kikosi changu,” alisema Nabi.
Pia, alisema katika mashindano hayo atatumia wachezaji wa timu za vijana.
Kocha huyo raia wa Tunisia alisema kuwa anapanga mikakati hiyo ili wachezaji wake ambao wametumika kwa muda mrefu waweze kupata muda wa kupumzika na kubaki katika ubora wao hasa katika mbio za kutafuta ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Licha ya Yanga, katika kundi A la michuano hiyo, zimepangwwa timu za Azam FC, Namungo, Yosso FC na Meli 4 City wakati kundi C likiwa na timu za Simba, Sallem View na Mlandege.
Na NASRA KITANA