RAIS Samia Suluhu Hassan, amebainisha kuwa, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya sh. bilioni 100 zitakazodhibiti kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini.
Kauli ya Rais imekuja mwezi mmoja tangu Waziri wa Nishati, January Makamba, ambapo Mei 10, mwaka huu, alitangaza bungeni jijini Dodoma, uamuzi wa serikali kutekeleza agizo la kiongozi huyo wa nchi la kutoa ruzuku ya sh. bilioni 100, ili kupunguza makali ya bei ya mafuta sokoni.
Akizungumza na mamia ya wananchi wa mji mdogo wa Bwanga, mkoani Geita, waliojitokeza kumlaki akiwa njiani kwenda mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi, Rais Samia alisema ruzuku hiyo ni endelevu hadi hali itakapokuwa nzuri.
“Tunajaribu kutoa ruzuku, kama mlisikia mwezi uliopita nilisema natoa ruzuku ya bilioni 100 ili kufidia kwenye mafuta, bei ishuke na mwezi huu bei zimeanza kushuka polepole.
“Tutaendelea kutoa hiyo ruzuku mpaka duniani kukae sawa, tutaendelea kukata bilioni 100 kila mwezi katika matumizi ya serikali, tuweke ruzuku katika mafuta mpaka bei zikae sawa, hiyo ni kupunguza makali ya mafuta, kwa hiyo zitakuwa zinashuka zinashuka mpaka tufikie bei zilivyokuwa,” alisema.
Kabla ya kueleza uamuzi huo wa serikali, Rais alitoa ufafanuzi wa chanzo cha kupanda kwa bei ya mafuta nchini na kwingineko duniani, kuwa ni uwepo wa machafuko katika mataifa ya Ukraine na Russia ambayo mojawapo ni mzalishaji mkubwa wa gesi.
Alisema gesi hutumiwa kwa kiasi kikubwa na nchi nyingi zilizoendelea barani Ulaya na Marekani, hivyo kutokana na kusimama kwa muda kwa uzalishaji, kumekuwa na uhitaji mkubwa wa mafuta, hali inayosababisha bei yake sokoni kupaa maradufu kote duniani ikiwemo Tanzania.
“Bei ya mafuta ikipanda, dizeli ambayo meli zinatumia kutuletea bidhaa bei yake nayo inapanda…,tulikuwa tunasafirisha kontena moja kwa dola 1,800 sasa hivi kontena moja la bidhaa likija kwenda ni dola 1,800 mpaka 1,900, kwa hiyo bidhaa hupanda bei pia kwa mtindo huo,” alifafanua Rais.
NAIBU WAZIRI NISHATI
Akifafanua uamuzi huo wa Serikali wakati akiwasalimia wananchi wa Biharamulo, Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, ambaye aliambatana na Rais Samia katika ziara hiyo, alisema uhalisia wa bei ya mafuta duniani, bado inapanda lakini hapa nchini serikali imeishusha.
“Waziri wa Viwanda amesema hapa, bei (kwa Biharamulo) ilikuwa lita kwa Shilingi 3,500 hadi shilingi 3,540, lakini leo ni sh. 3,200, sio kwamba yameshuka, Rais Samia ameyashusha na asingeyashusha, yangekuwa zaidi ya shilingi 3,700, kwa kuwa kule yanakotoka bei inaendelea kupanda,” alisema Byabato.
TAMKO LA SERIKALI BUNGENI
Akizungumza bungeni Mei 10, mwaka huu, Waziri January alisema uamuzi wa kutoa ruzuku hiyo, ulifikiwa na Rais Samia, ikiwa ni moja ya hatua za kusaidia kupunguza gharama za maisha kwa Watanzania, ambao siku za hivi karibuni, walishuhudia bei za bidhaa na huduma mbalimbali zikipaa.
“Ruzuku hii inatolewa kwa kupunguza matumizi ya Serikali katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2021/22.
Kutolewa kwa ruzuku hii, hakutagusa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea,” alisema January katika hotuba yake bungeni.
Kabla ya kauli yake, Waziri huyo alipewa wiki moja na Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson, kueleza hatua zinazofanywa na Serikali kukabiliana na kuongezeka kwa gharama za maisha kulikosababishwa na kupaa kwa bei za mafuta ya katika soko la Dunia.
Makamba alisema kwamba, Serikali imeomba mkopo kutoka Benki ya Dunia (World Bank), na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kwa ajili ya kuleta ahueni katika bei za mafuta na bidhaa nyinginezo zinazogusa maisha ya watu.
“Mchakato wa kuchukua mkopo huo, uko mbioni kukamilika na ahueni katika kupanda kwa bei za bidhaa, itapatikana katika mwaka ujao wa fedha,” alisema Waziri Makamba.
Na WILLIAM SHECHAMBO