Na Mwandishi Wetu, Singida
SERIKALI imewaasa wafungwa nchini kuzidisha kufanya ibada na kuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu ili wakitoka waende kuwa raia wema na kukamilisha ndoto walizokuwa nazo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Chilo, katika kikao cha ndani, kilichohusisha wafungwa na mahabusu katika Gereza la Wilaya ya Sindida Mjini.
Naibu Waziri, pia alipata fursa ya kuwasikiliza wafungwa waliotoa maoni, mapendekezo na changamoto mbalimbali walizokuwa nazo, ikiwemo kuchelewa kwa upepelezi wa kesi zao.
“Rais anawategemea sana, hususan vijana, na Taifa hili linawategemea sana, hapa naona vijana mko wengi, vijana ndio nguvu kazi ya Taifa, sasa endeleeni kuwa raia wema, ukitoka hapa kifungoni nenda kawe raia mwema.
“Mkitoka hapa nendeni mkaendeleze ndoto zenu, fanyeni ibada muombeni Mwenyezi Mungu sana, huwezi kujua ukitoka hapa utaenda kuwa nani, maana historia inatuonyesha wako watu mbalimbali walikuwa wafungwa, lakini walivyomaliza vifungo vyao, walikwenda kuwa viongozi wakubwa tu,” Naibu Waziri Chilo
Akisoma taarifa ya gereza mbele ya Naibu Waziri, Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Singida, alisema katika gereza hilo, kuna shughuli mbalimbali za uzalishaji, ikiwemo kilimo cha mahindi, maharage, mbogamboga, ufyatuaji wa tofali, ufugaji wa samaki na ujenzi wa nyumba za makazi ya askari.