Na MWANDISHI WETU
SAA chache kabla ya kushuka dimbani kuivaa na Pyramids FC ya Misri, Kocha wa Namungo, Hemed Morocco, amesema kikosi chake kipo tayari kwa kipute.
Namungo itapepetana na Pyramids katika mchezo wa pili wa makundi kuwania Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika leo Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Timu hiyo itashuka dimbani huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Raja Casablanca kwa bao 1-0.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika mkutano wa maandalizi ya mchezo huo, kocha wa timu hiyo alisema kikosi chake ameiandaa vyema timu kutumia uwanja wa nyumbani ili kupata matokeo mazuri.
Morocco alisema kuwa wachezaji wanatambua umuhimu wa mechi hiyo na wameahidi kulipa kisasi baada ya kupoteza pambano lililopita.
“Tuna kila sababu ya kupata ushindi katika dimba la nyumbani, tumepoteza mechi ya awali kwa bahati mbaya lakini hii ni lazima tutavuna pointi,” alisema.
Alisema katika mechi ya awali, timu yake ilifanya makosa kwenye eneo la ulinzi lakini amerekebisha kasoro na timu ipo tayari kwa mechi.
Nahodha wa timu hiyo, Hamis Mugunya, alisema ana imani na wenzake na anakubali ushindani mkubwa uliopo kwa wapinzani wake na kuahidi kuzitumia vyema dakika 90 kupata ushindi wa nyumbani.
“Tutahakikisha tunashinda mchezo huu ili kuendelea kulinda heshima ya nchini yetu, naamini hata wawakilishi wenzetu katika mashindano ya kimataifa , Simba, watafanya kweli leo (jana) na kutupa nguvu zaidi,” alisema Mungunya.
Namungo ilitinga hatua ya makundi baada ya ushindi wa jumla ya mabao 7-5 baada ya kushinda mchezo wa kwanza dhidi ya Agosto ya Angola katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamanzi jijini Dar es Salaam kabla ya kukubali kichapo cha mabao 3-1 kwenye mchezo wa marudiano uliochezwa Dar es Salaam pia.
Timu hiyo ipo Kundi D pamoja na Raja Casablanca ya Morocco, Pyramids FC ya Misri na Nkana FC ya Zambia.
Hadi sasa, Namungo ina uhakika wa kuvuna dola 275,000 (zaidi ya sh. milioni 600 za Kitanzania) endapo itamaliza michezo ya kundi ikiwa nafasi ya tatu na nne na kama itamaliza ikiwa nafasi ya pili au ya kwanza itazoa zaidi ya sh. milioni 800.