SERIKALI imetangaza punguzo la asilimia 33 ya bei ya mbuzi na kondoo waliopo katika Ranchi za Taifa (NARCO) katika msimu huu wa sikukuu ili kuhamasisha wananchi kula nyama na kuongeza wigo wa soko la ndani.
Akitangaza punguzo hilo Ofisa Masoko wa NARCO, Immanuel Mnzava, amesema serikali imeamua kutoa ofa ya krismas na mwaka mpya kwa wananchi wake ambapo mbuzi 3,000 na kondoo 1,000 watauzwa kwa bei ya punguzo.
Amesema bei hiyo itakuwa katika ranchi za Kongwa (Dodoma), Ruvu (Pwani), Mkata (Morogoro), West Kilimanjaro (Kilimanjaro), na Missenyi (Kagera).
“Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kutoa ofa ya krismas na mwaka mpya kwa wananchi wake ambapo ofa hii inalenga kuhamasisha ulaji wa nyama ya mbuzi na kondoo hapa nchini na kuongeza soko la bidhaa hiyo ndani ya nchi,”alisema
Ameeleza kuwa awali mbuzi mmoja katika ranchi hizi alikuwa anauzwa hadi sh. 150,000 lakini kutokana na punguzo hili sasa watauzwa kwa sh. 120,000 hadi 100,000, kwa mbuzi na kondoo ambaye akichinjwa anatoa kilo 15 hadi 20.
Kwa mujibu wa Ofisa huyo amesema takwimu zinaonyesha kuwa ulaji wa nyama ya mbuzi na kondoo hapa nchini bado uko chini ikilinganishwa na ulaji wa nyama ya ng’ombe ambao unaongezeka kila mwaka.



























