Na SALVATORY NTANDU, KAHAMA
MIGOGORO ya kifamilia, ndoa na mimba za utotoni mkoani Shinyanga, zimetajwa kuchangia ukiukwaji wa haki za watoto na kusababisha madhara ya kiafya, ikiwemo vifo vitokanavyo na uzazi.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela, wakati akisoma taarifa kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, yaliyofanyika katika Halmashauri ya Ushetu.
Alisema vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, vinaendelea kushamiri mkoani Shinyanga na bado jamii zinaendelea kukumbatia mila na tamaduni potofu, ambazo zinachangia kuongezeka kwa matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Msovela, alieleza kuwa endapo hatua za haraka zisipochukuliwa, zinaweza kumkwamisha mwanamke katika kutimiza ndoto zake kielimu na kiuchumi.
“Vijijini bado kuna wazee wanaoa watoto chini ya umri wa miaka 18, huku baadhi ya wazazi wakitajwa kushiriki kuozesha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, ili waweze kupatiwa fedha au mifugo, bila ya kujua athari zinazoweza kuwapata pindi wanapoolewa,”alisema.
Alifafanua kuwa ndoa hizo zinaweza kuwa kichocheo cha watoto kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali ya ngono kwa sababu wengi wao hawana uelewa kuhusu elimu ya afya ya uzazi.
Mkazi wa Kijiji cha Salawe, Esta Mwandu, alisema kuna waganga vijijini wanaopiga ramli chonganishi ili kuwashawishi wanaume kufanya mapenzi na watoto wenye umri mdogo, waweze kupata mali.
Alisema vitendo hivyo vinasababisha watoto chini ya umri wa miaka 18, kupata mimba na wengine kuambukizwa magonjwa ya zinaa.
“Tabia hii imeshamiri vijijini, wanafunzi wanabakwa na wanaume, lakini kesi hizi zinamalizwa chini chini, tunaiomba serikali kwa kushirikiana na mashirika, ikiwemo Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake Tanzania (WFT), kutoa elimu dhidi ya mila hizo potofu,” alibainisha.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, aliwataka wazazi na walezi kupiga vita vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake.
Aliongeza kuwa katika kufikia usawa wa asilimia 50 kwa 50, jamii inapaswa kubadilika kwa kuacha mfumo dume na mila kandamizi dhidi ya wanawake na watoto, ili kutoa fursa ya kupata haki sawa katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.