Na Samson Chacha, Rorya
MKAZI wa Kijiji cha Kitembe, Kata ya Kitembe, Tarafa ya Girango, wilayani Rorya, Mkoa wa Mara, Peter Ochieng (53), amejeruhiwa sehemu mbalimbali baada ya kupigwa marungu kisha kukatwakatwa mapanga na ndugu zake wawili.
Watuhumiwa hao, Omolo Oyugi na Kwaga Oyugi, wanadaiwa walimvamia Ochieng, usiku wa saa nane, wakitaka awapatie fedha alizouza ng’ombe wake wawili.
Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, ACP William Mkonda, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba, mtuhumiwa Omolo
amekamatwa huku msako ukiendelea kwa mtuhumiwa wa pili.
Akisimulia mkasa huo kwa waandishi wa habari juzi, katika Kijiji cha Kitembe, Wilayani Rorya, Ochieng, alidai Januari 4, mwaka huu, aliuza ng’ombe wake wawili kwenye mnada wa Randa, kwa sh. milioni 1.2.
“Ndugu zangu waliniona nikiuza mifugo hiyo na kupokea fedha hizo, nilirejea nyumbani kwangu, lakini usiku saa nane nilisikia mlango wa nyumba ukivunjwa. Nilijaribu kupiga kelele za kuomba msaada kwa majirani, lakini wahalifu hao, ambao ni ndugu zangu, walianza kunikata kwa mapanga. Walinikata mapanga kichwani, mgongoni, kifuani na mikono yote miwili huku wakiomba fedha nilizouza ng’ombe,” alieleza.
Ochieng, alidai baada ya watuhumiwa kusikia watu wanaanza kujitokeza kutoa msaada, walikimbia na kumuacha akiwa amejeruhiwa sehemu mbalimbali.
“Mke wangu na majirani walinichukua kunipeleka Hospitali ya Shirati, kupatiwa matibabu, ambapo nililazwa huko kwa zaidi ya wiki tatu, hali yangu bado siyo nzuri, nimeambiwa niende Hospitali ya Rufaa Bugando,” alidai.
Alisema hadi sasa bado hana uwezo wa kutembea kwa sababu ya kukatwa mapanga karibu na uti wa mgongo huku mikono yake ikiwa haifanyikazi.
“Hali yangu ni mbaya sijiwezi. Nilifungua kesi Kituo cha Polisi Utegi, yenye RB namba IR/UTG/5/2021, mtuhumiwa mmoja Omolo, amekamatwa bado wa pili Kwaga. Usiku anapita nje ya nyumba yangu kutoa vitisho kuwa atanitoa roho yangu na familia yangu,” alidai.