WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Fautine Ndugulile amewataka wananchi, wafanyabiashara, wajasiriamali na wenye viwanda kutumia mfumo wa duka mtandao ili kuuza na kununua bidhaa ndani na nje ya nchi.
Amesema mfumo wa duka mtandao utasaidia kuimarisha masoko kimataifa, ambapo Shirika la Posta lina mtandao wenye kukidhi mahitaji ya dunia ya matumizi ya mifumo ya kidigitali.
Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, katika Maonyesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (DITF), katika utiaji saini makubaliano ya uzinduzi wa duka mtandano, kati ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade) na Shirika la Posta.
Waziri Ndugulile alisema wakati umefika wa kupanua wigo wa matumizi ya mifumo ili kufanya biashara kimataifa na kujiletea maendeleo. Alilitaka Shirika la Posta kuimarisha matumizi ya mfumo huo, ili kukidhi mahitaji yaliyopo na kuwataka wananchi wachangamkie fursa hiyo.
“Kauli mbiu ya maonyesho ni Uchumi wa Viwanda, Ajira kwa Vijana na Biashara Endelevu, uzinduzi wa duka mtandao utasaidia kuimarisha mauzo ya bidhaa ili kufikia lengo la biashara endelevu kimataifa,”alisema.
Alisema wizara itaendelea kutumia fursa zilizopo katika kuunganisha masuala ya habari na tekenolojia, ili kuwezesha maendeleo ya kiuchumi na matumizi bora ya TEHAMA, yatafungua milango ya masoko kwa mauzo ya wajasiriamali.
“Tumenunua magari matano na tutaongeza mengine, lengo ni kuweza kusafirisha bidhaa kwa wakati, hivyo wafanyabiashara ,wajasiriamali, wenye viwanda na jamii watumie fursa hiyo kwenda na mahitaji ya dunia katika matumizi ya kimfumo,”alisema.
Ndugulile aliongeza “Wakati umefika wa kuboresha matumizi ya taarifa binafsi, hakuna haja unaenda polisi unaulizwa kabila unaenda hospitali unaulizwa dini yako inahusiana nini,”.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, alisema taifa limekuwa na matumizi mengi ya mitandao ambayo hayana maslahi katika kukuza uchumi.
Profesa Mkumbo alisema ni muhimu kutumia matumizi ya kidijitali kuimarisha uchumi na kufikia malengo ya kimkakati na wizara yake itatumia uzinduzi wa duka hilo kuimarisha sekta ya biashara, kwa kuunganisha nguvu katika kukuza maendeleo.
MARIAM MZIWANDA Na REHEMA MAIGALA



























